NLD kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Doyo awa mgombea urais

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:37 PM Apr 11 2025
NLD kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Doyo awa mgombea urais
Picha: Mpigapicha Wetu
NLD kushiriki Uchaguzi Mkuu 2025, Doyo awa mgombea urais

Chama cha National League for Democracy (NLD) kimemtangaza rasmi Katibu Mkuu wake, Doyo Hassan Doyo, kuwa mgombea wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Uamuzi huo umetangazwa kufuatia kukamilika kwa mchakato wa ndani wa chama, uliolenga kuwapitisha wagombea wa nafasi za juu kwa ajili ya uchaguzi huo. Sambamba na Doyo, chama hicho pia kimemteua Mfaume Khamis kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya NLD.

Taarifa rasmi iliyotolewa na Kitengo cha Habari cha NLD kwa vyombo vya habari imeeleza kuwa uteuzi huo umezingatia vikao halali vya chama, taratibu za kikatiba, pamoja na mapendekezo ya wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi.

“Tunaamini kwamba viongozi wetu hawa ni mfano wa uongozi bora na wenye dira ya kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania. NLD imejipanga kuendeleza misingi ya demokrasia, uzalendo, haki na maendeleo jumuishi kwa kila Mtanzania,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa kutangaza mgombea wake, NLD kimekuwa chama cha pili kufanya hivyo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025, kikifuatiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kilimtangaza mapema mwaka huu Rais wa sasa Dk. Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wao wa urais kwa awamu ya pili.