Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mnarani iliyopo mkoani Mwanza Dismas Hamaro amesema nusu ya wanafunzi wote wanaosoma shuleni hapo wanaketi chini kwa kukosa madawati ya kukali hali inayosababisha usumbufu wakati wa masomo.
Hamaro amebainisha hayo jana wakati akipokea viti na madawati 80 kwa ajili ya wanafunzi wa awali vilivyotolewa na Asasi isiyo ya kiserikali ya The Desk and Chair Foundation Tanzania.
Amesema shule hiyo imekuwa ikikabiliwa na upungufu mkubwa wa madawati kwa ajili ya wanafunzi ambapo nusu ya wanafunzi kwa shule nzima walikuwa wakikaa chini jambo lililochangia kushindwa kujifunza kwa ufanisi na kuchangia wanafunzi kutohudhuria masomo.
“Shule yetu ina wanafunzi 818, nusu ya wanafunzi walikuwa wakikaa chini msaada huu umesaidia wanafunzi 80 kati ya 158 wa darasa la awali pekee watakaa kwenye meza na viti na hivyo,” amesema Hamaro.
Aidha amesema kati ya hao watakaokosa dawati ni wanafunzi 78 na kuhahidi kutayatunza vyema ili viendelee kuwa chachu ya kujifunzia na kuimarisha umahiri wa wanafunzi kusoma na kuandika.
Akimkabidhi madawati hayo Mwenyekiti wa asasi hiyo Sibtain Meghjee amesema lengo la kutoa msaada huo ni kuhakikisha wanafunzi hao wanapata nafasi ya kujifunza katika mazingira ya kisasa na ya kiustawi.
Amesema wanaamini kuwa madawati hayo yatasaidia kuboresha hali ya masomo na kutoa nafasi kwa watoto hao kuwa katika mazingira bora ya kujifunzia.
"Tunawaomba madawati haya yatunzwe kwa uangalifu na yatumike kwa manufaa ya wanafunzi wa shule hii, huu ni mchango wa moja kwa moja kutoka kwenye taasisi yetu kama sehemu ya juhidi zetu za kuboresha mazingira ya kujifunza na kusaidia maendeleo ya elimu katika shule mbalimbali" amesema Meghjee.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED