Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limetangaza limejipanga kikamilifu kuimarisha ulinzi katika kipindi chote kinachoelekea Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), ambayo kwa mwaka huu itaadhimishwa kitaifa katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 23, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Amoni Kakwale, amesema vyombo vya dola vipo tayari kuhakikisha usalama na amani vinatawala wakati wote wa maandalizi na siku ya tukio.
"Tumejipanga vyema kuhakikisha wananchi wanasherehekea kwa amani na utulivu. Kwa mtu yeyote atakayepanga kufanya uhalifu, awahi kujua kuwa tutamkamata na atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” amesema Kamanda Kakwale.
Ameongeza kuwa jeshi hilo litashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuhakikisha wageni wote waalikwa, viongozi wa serikali na wananchi kwa ujumla wanakuwa salama kabla, wakati na baada ya maadhimisho hayo muhimu.
Aidha, Kamanda Kakwale ametoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuzuia uhalifu na kuwabaini watu wenye nia ovu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED