Wakazi wa Kijiji cha Nyasamba, Wilaya ya Kishapu, sasa wamepata afueni baada ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutatua tatizo la maji lililosababishwa na kuharibika kwa pampu ya kisima kirefu. Huduma hiyo ilikuwa imesimama kwa zaidi ya siku mbili.
Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wananchi wamesema kuwa kutokana na tatizo hilo walilazimika kutumia maji ya mabwawa ambayo si salama kwa afya zao.
Mmoja wa wananchi hao, Leah Samweli, amesema:
"Tulipata shida kubwa kutokana na ukosefu wa maji salama na kulazimika kutumia maji yasiyo safi. Tunashukuru RUWASA kwa hatua ya haraka kurejesha huduma hii. Ombi letu kwa serikali ni kutuletea Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria ili tuondokane kabisa na changamoto hii ya kukatika kwa maji kila pampu inapoharibika."
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyasamba, Martin Kafumu, amesema kijiji hicho chenye takribani kaya 800 kilikuwa katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko kutokana na ukosefu wa maji salama. Ameishukuru RUWASA kwa hatua ya kurejesha huduma hiyo muhimu.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kishapu, Mhandisi Dickson Kamazima, amesema tatizo la maji lilitokana na kuharibika kwa pampu ya kisima kirefu kinachohudumia matangi ya Bubiki na Nyasamba.
"Kwa sasa tumefunga pampu mpya na huduma za maji safi na salama zimerudi kama kawaida," amesema Mhandisi Kamazima.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED