Mgombea urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameahidi kujenga mji wa Uyole kuwa Kituo Kikubwa cha Kimkakati cha Biashara cha Kimataifa.
Mwalimu amesema Kituo hicho kitatumika kuleta wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania kwa kuwa mji huo unapakana na nchi jirani. Amesema hayo leo akiwa Uyole mkoani Mbeya akiendelea na kampeni za kuomba kuchaguliwa kuwa Rais wa Tanzania ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.
Amesema kupitia mwingiliano huo wa kibiashara, na kupitia Kituo hicho ambacho kitajegwa, kitatumika kuzalisha fursa nyingi za kiuchumi. "Kama kitajengwa Kituo kikubwa hapa, si rahisi mfanyabiashara kutoka nchi jirani kwenda mpaka Dar es Salaam au akatoka mkoa huu au mikoa ya jirani akaenda mpaka Dar es Salaam akaacha kuja hapa,"amesema Mwalimu.
"Tutatengeneza Uyole ya kisasa kuanzia miundombinu ya kimkakati na Kituo kikubwa cha Kimataifa cha kimkakati na Tanzania ikijengwa kwa mtindo huo hakutakuwa na sababu ya kwenda kubanana sehemu moja, na tutatengeneza uchumi ambao umetawanyika kila pembe ya nchi."
"Yaani kila pembe ya nchi kutatengenezwa matajiri, magorofa yanayojengwa Dar es Salaam kutakuwa na uwezo wa kuyajenga maeneo mengine pia na hata maeneo ya starehe yanayojengwa katika miji hiyo mikubwa ya Dar es Salaam, itajengwa pia na mikoa ya kila pembe ya nchi, vivyo hivyo hata bata litaliwa kila kona ya nchi."
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED