Samia: Ruzuku imekuza uzalishaji korosho

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:28 PM Sep 26 2025
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan

Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Samia Suluhu Hassan amesema hatua ya Serikali yake kutoa ruzuku ya mbolea kwa zao la korosho, kumeongeza uzalishaji wa zao hilo na kuifanya Tanzania kuwa nafasi ya pili Afrika.

Dk Samia ameyasema hayo leo, Ijumaa Septemba 26, 2025 alipozungumza na wananchi wa Mtwara Mjini mkoani Mtwara katika mkutano wa kampeni za urais, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi.

“Nchi yetu Tanzania ni ya pili kwa Afrika katika kuzalisha korosho, wanaotupita ni nchi inaitwa Ivory Coast wa pili ni sisi. Kwa hiyo tutaendelea kuweka jitihada ili twende sambamba na nchi hiyo ambayo sasa inaongoza," amesema.

Kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wake pekee, amesema Serikali imetoa ruzuku ya pembejeo yenye gharama ya Sh726 bilioni kwa ajili ya kugawa mbolea za ruzuku nchini kote.

“Kila mwaka tunatumia kiasi cha Sh152 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya mbolea na pembejeo za kilimo, fedha ambayo ingetoka mfukoni kwa wakulima. Lakini tumeibakisha mifukoni mwao Serikali tunagawa kwa ruzuku nusu bei, lakini vitu vingine bure,” amesema.

Amesema hatua hiyo imesababisha uzalishaji wa korosho ukue kutoka tani 118,811 mwaka 2020/21 zilizouzwa kwa thamani ya Sh265 bilioni hadi tani 330,505 mwaka 2025 zilizouzwa kwa Sh1.9 trilioni.