CHAMA cha Demokratic-DP kimemsimamisha uanachama Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Peter Agaton Magisiri pamoja na wanachama wengine saba kwa tuhuma za kumuunga mkono mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dk. Husein Ally Mwinyi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mwenyekiti wa chama hicho ambae pia ni mgombea wa Urais wa chama cha DP, Juma Mluya wakati akizungumza na waandishi wa habari Wilayani Kahama mkoani Shinyanga, baada ya kuahirisha mkutano wake kufuatia kuwa na vikao mbalimbali kwa njia ya mtandao kutokana na kauli za makamu mwenyekiti zenye lengo la kuvuruga msimamo wa chama.
"Hatuwezi kuwavumilia viongozi wasio wadilifu wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti ambae sio msemaji wa chama kwa mujibu wa katiba yetu, Mwenyekiti ndio msemaji ambae ndio mimi, hivyo nimemuagiza Katibu mkuu kuwaandikia barua ya kuwasimamisha uongozi wakiwemo wajumbe na wanachama walioshiriki kwenye kikao hicho"Aliongeza Juma.
Aliongeza kuwa"Katiba ya chama hiki katika ibara ya 13(2)inasema Mwenyekiti wa chama ndio mlinzi wa Katiba na Msemaji wa chama hivyo taarifa ya Makamu huyu ipuuzwe kwani sio msimamo wa chama na nimepata mshtuko wa moyo hivyo ninaahirisha ziara katika mkoa huu"
Aidha Juma alisema, kufuatia kauli hiyo amelazimika kuahirisha ziara katika mkoa wa shinyanga ili aweze kupumzika kwani jambo hilo amedai limemuathiri kiafya na baada ya mapumziko ya siku mbili kuanzia sasa ataendelea na ziara zake kwa mujibu wa ratibu ya tume ya uchaguzi nchini.
Kadhalika alisema, lengo la chama ni kushika dola ili kukwamua watanzania kwa kupata huduma bora katika sekta za afya, elimu, kilimo na mambo mengine muhimu hivyo kitendo cha viongozi hao kwenda kinyume na msingi ya chama ni sehemu ya kukikwamisha chama kisiweze kushinda nafasi ya urasi na nyingine za ubunge na udiwani.
Hata hivyo aliwataja waliosimamishwa uachama kuwa ni pamoja na Peter Agatoni Msgasira ambae ni Makamu Mwenyekiti wa chama Zanzibar, Zainabu Juma Khamisi, Mkude John Mkude, Salma Mateo Petro, Juma Ramadhani Kidawa, Mariam Brash Maseka, Makame Omani Makame, Leonard Damiani Mkoga, kuwa hapo ni wajumbe wa sekretarietI na baadhi ya wanachama.
Mgombe huyo alipaswa kufanya mkutano wake wa kuomba kura kwa wananchi septemba 26 mwaka huu katika viwanja vya kata ya Mhongolo halmashauri ya Manispaa ya Kahama akitokea mkoani Kigoma, lakini ameshindwa kufanya mkutano huo kutokana na kauli za mgombea urais zanzibar za kumuunga mkono mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi Dk. Husein Ally Mwinyi kuwa sio agizo la chama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED