Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo, amewataka vijana waliomaliza mafunzo ya kijeshi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha 843KJ, kuhakikisha wanatumia mitandao ya kijamii kwa manufaa yao binafsi na kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya Operesheni Okoa Nishati Safi, DC Moyo alisema kuwa matumizi yasiyo sahihi ya mitandao yamekuwa changamoto kwa vijana wengi wa Kitanzania, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
"Bando mnaweka, lakini wengi hamjui kutumia mitandao kwa maendeleo yenu. Badala ya kuhamasisha chuki na migogoro, tumieni mitandao kujifunza, kuelimishana na kulinda amani ya nchi," alisisitiza DC Moyo.
Aidha, aliwataka vijana hao kuwa mabalozi wa amani na elimu sahihi kuhusu matumizi bora ya mitandao ya kijamii katika jamii wanazotoka, akieleza kuwa Tanzania inahitaji kizazi chenye uzalendo na uwezo wa kutumia teknolojia kwa njia chanya.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana waliomaliza mafunzo hayo kupitia Operesheni Okoa Nishati Safi, walieleza kuwa wako tayari kushiriki kikamilifu katika kuilinda nchi na kueneza elimu kuhusu matumizi salama na yenye tija ya mitandao ya kijamii.
"Tumejifunza nidhamu, uzalendo, na sasa tupo tayari kuwa walinzi wa amani na kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya mitandao," alisema mmoja wa wahitimu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED