Salum Mwalimu: Serikali yangu ni marufuku Ma-RC na Ma-DC machawa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 03:24 PM Sep 27 2025
Salum Mwalimu: Serikali yangu ni marufuku Ma-RC na Ma-DC machawa
PICHA: ELIZABETH ZAYA
Salum Mwalimu: Serikali yangu ni marufuku Ma-RC na Ma-DC machawa

MGOMBEA Urais wa Chama cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA), Salum Mwalimu amesema serikali yake haitataka wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa 'machawa' bali viongozi wachapa kazi na wenye mipango kazi ya kuwaondolea wananchi wake umasikini.

Mwalimu ametoa kauli hiyo leo kwenye mkutano wa kampeni Uyole mkoani Mbeya. Amesema RC, DC na viongozi atakaowataka kwenye serikali yake ni wenye mipango mikakati ya kuondoa umasikini kwenye maeneo yao ya kazi.

Kadhalika, amesema viongozi wote wasiowajibika kwenye serikali yake, hatowafukuza bali watakuwa wanajifukuza wenyewe kazini. "Itakuwa ni serikali ya mpela mpela, yaani sitataka Wakuu wa Wilaya au Wakuu wa mikoa machawa, nitataka wanaofanya kazi, hakuna kukaa ofisini eti umevaa na tai unakula kiyoyozi, itakuwa ni mwendo wa kazi, kwenda mitaani kusikiliza matatizo ya wananchi  na kutafuta majawabu.

"Tutakwenda mitaani kutafuta namna gani tunatengeneza ajira za vijana, namna gani tunainua uchumi wa nchi yetu, kwa hiyo haitakuwa nchi ya machawa, itakuwa ya watu wa kazi na asiyefanya kazi atajifukuzisha kazi mwenyewe,"amesema Mwalimu.

"Hivi wewe utakaa ofisini eti unapigwa na kiyoyozi, una raha gani wakati wananchi wako wanateseka huko, lazima tuwe na viongozi wenye fikra mpya na watakaojitoa maisha yao kusaidia nchi hii kuitoa hapa ilipo kuipeleka mbele."