Vijiji vya Butibu na Igunda vyapewa hati miliki za kimila kuondoa migogoro ya Ardhi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 02:59 PM Sep 27 2025
Mwenyekiti wa kijiji cha Iguda halmashauri ya Ushetu Isaya Kibela akikabidhiwa daftari la ardhi la kijiji la hati miliki ya kimila, na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Deus Kakulima
PICHA; SHABAN NJIA
Mwenyekiti wa kijiji cha Iguda halmashauri ya Ushetu Isaya Kibela akikabidhiwa daftari la ardhi la kijiji la hati miliki ya kimila, na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Deus Kakulima

WAKAZI 1,022 wa vijiji vya Butibu na Igunda Halmashauri ya Ushetu mkoani Shinyanga, wamepatiwa hati miliki za kimila ili kuimarisha umiliki halali wa ardhi na kukabiliana na migogoro ya ardhi inayolikumba Taifa kwa muda mrefu.

Akikabidhi hati hizo leo Mkurugenzi wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Usimamizi na Uratibu kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya matumizi ya ardhi Jonas Masingija amesema, itaendelea kutatua migogoro ya ardhi vijijini kwa kutoa hati hizo.

 Amesema, mpaka sasa wameshatoa hati miliki za kimila katika vijiji 4,729 na kubaki vijiji 7,604 kutimiza idadi ya vijiji 12,333 nchi nzima na uwepo wake umesaidia kuimarika kwa salama za miliki kwa wananchi hususani wale wanaoishi katika maeneo husika.

 Masingija amesema, utoaji wa hati hizo unalenga pia kuongeza thamani ya ardhi nchini, kuwakwamua wananchi katika wimbi la umasikini pamoja na kuweka suluhu ya kudumu ya migogoro ya ardhi iliyoota mizizi katika maeneo mbalimbali na wanaendelea kuanda ili vijiji vingine viweze kupata.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Denis Kakulima amesema, wataendelea kutenga fedha kupitia mapato ya ndani kila mwaka ili wananchi wa vijiji vyote 112 wanafikiwa na kuandaliwa hati hizo kwani mpaka sasa ni vijiji 36 tu vilivyopata na kubaki vijiji 76.