Watu wasioona kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wamenufaika na mafunzo yaliyotolewa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kwa lengo la kuwawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya kazini.
Mafunzo hayo ya siku moja ambayo yametolewa kwa wanachama 50 wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TAB) yamehusisha mada mbalimbali zikiwemo utambuzi na udhibiti wa vihatarishi vya usalama na afya pamoja na misingi ya huduma ya kwanza mahali pa kazi.
Washiriki wa mafunzo hayo wanajihusisha na shughuli mbalimbali zikiwemo ushonaji, kilimo, ufugaji, uzalishaji wa bidhaa zikiwemo sabuni na biashara ndogondogo.
Akifungua mafunzo hayo, Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi anayoiongoza inatambua thamani na mchango wa watu wenye ulemavu katika kujenga uchumi wa Taifa jambo ambalo limepelekea mafunzo hayo kuandaliwa pamoja na mafunzo mengine ambayo OSHA imekuwa ikayatoa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu.
“Niwapongeze washiriki wote wa mafunzo kwa kuitikia mwaliko wa kushiriki mafunzo haya muhimu kwenu kwani ni dhahiri kuwa ulemavu ni hali tu ambayo haipaswi kuwa kikwazo kwenu kushiriki katika shughuli za kiuchumi,” amesema Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:
“Sambamba na mafunzo haya, tutawapatia vifaa saidizi zikiwemo fimbo nyeupe, karatasi za nukta nundu pamoja na vitabu maalum vya nukta nundu vyenye maudhui ya mafunzo ya usalama na afya kwa ajili ya rejea zaidi.”
Aidha, Mwenda ameahidi kuwa mafunzo ya usalama na afya kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu yatafuatiwa na zoezi la kutembelea maeneo yao ya kazi kwa ajili ya kutathmini mazingira ya kazi ili kushauri namna sahihi ya kuboresha mazingira hayo.
Awali, akiwasilisha salamu za Jumuiya ya Wasiiona Tanzania, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Omary Itambu, ameipongeza OSHA kwakuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha watu wasioona pamoja na makundi mengine ya watu wenye ulemavu.
“Tunaiomba OSHA kuendeleza utamaduni huu wa kutujali watu wenye ulemavu. Kwa niaba ya washiriki wenzangu niwahakikishie OSHA kuwa mafunzo mliyotupatia si tu yatakwenda kuimarisha afya na usalama wetu bali yatatusaidia sana kuongeza thamani ya huduma na bidhaa tunazozalisha,” amesema Itambu.
Aidha, Itambu ametoa wito kwa washiriki wenzake wa mafunzo kuwa mabalozi wazuri wa OSHA ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wenzao ambao hawakupata fursa ya kushiriki mafunzo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki wengine wa mafunzo, Mratibu wa Idara ya Vijana wa Jumuiya ya Wasioona,Bakari Hassan, amesema jambo lililofanywa na OSHA ni la kuigwa na Taasisi nyingine za kiserikali na zisizo za kiserikali, akisisitiza kwamba mafunzo hayo na vifaa saidizi walivyopewa vitarahisisha utendaji na kuongeza tija katika shughuli zao za kila siku.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED