UVCCM Kagera yasisitiza uwajibikaji kwa viongozi vijana

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 12:31 PM Apr 11 2025
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhani, ametoa wito kwa viongozi wa jumuiya hiyo katika ngazi zote kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa bidii na uwajibikaji ili kuendana na matarajio ya vijana waliowaamini na kuwachagua katika nafasi zao za uongozi.

Akizungumza na wajumbe wa Baraza la UVCCM Wilaya ya Muleba, ambao ni viongozi wanne kutoka katika kila kata miongoni mwa 43 zinazounda wilaya hiyo, Faris aliwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kuonyesha uadilifu na uzalendo katika nafasi walizonazo.

“Tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kwa uwazi ili kuzitendea haki nafasi tulizopewa. Huo ndiyo msingi wa kulinda imani ya vijana waliotuchagua,” alisema.

Aidha, alisisitiza kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia yanapaswa kuwa nyenzo ya kusaidia viongozi vijana kuonesha kwa uwazi shughuli wanazozifanya, muda wanaozifanya na mahali zinapotekelezwa.

“Siasa siyo mchezo wa jando na unyago. Ni kazi ya kuwahudumia watu, siyo jambo la kufanyika kwa siri. Hivyo, tutumie teknolojia kuweka wazi shughuli zetu kwa wananchi,” aliongeza.

Mwenyekiti huyo alihitimisha kwa kuwataka viongozi hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha mshikamano, maadili na uzalendo kwa vijana wengine ili kuhakikisha UVCCM inaendelea kuwa nguzo imara ya Chama Cha Mapinduzi mkoani Kagera.