UVCCM yawataka vijana wawe wazalendo na nchi yao

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 02:05 PM Apr 11 2025
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Sakala, akizungumza mara baada ya kuzindua Shina la Mama Kata ya Masekelo.
Picha: Marco Maduhu
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Sakala, akizungumza mara baada ya kuzindua Shina la Mama Kata ya Masekelo.

Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imewataka vijana kote nchini kuwa wazalendo na kuilinda amani ya nchi, wakikumbushwa kuepuka kutumiwa na wanasiasa kwa nia ya kuvuruga utulivu uliopo.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 10, 2025, wakati wa ziara ya uzinduzi wa Mashina ya Mama katika Kata za Masekelo na Ndala, pamoja na mikutano ya hadhara iliyolenga kuhamasisha wananchi na wanachama wa CCM kujiandaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza katika mikutano hiyo, Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Samson Suleiman, alisema uzalendo ni nguzo muhimu ya kulinda amani ya nchi na kuwataka vijana wasikubali kuwa chombo cha vurugu kisiasa.

“Amani yetu imejengwa kwa gharama kubwa na uongozi wa awamu zote, hivyo vijana wanapaswa kuilinda kwa moyo wa kizalendo na si kutumiwa kuivuruga,” alisema Suleiman.

Naye Katibu wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Naibu Katalambula, alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha misingi ya demokrasia nchini.

“Vyama vya siasa vina wajibu wa kutumia demokrasia hiyo kwa tija, si kuitumia kama mwanya wa kuvuruga amani ya nchi,” alisisitiza Katalambula.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abdulaziz Sakala, alisema kuwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM kwa asilimia 100 chini ya Rais Samia, UVCCM wamezindua kampeni ya Mama Full Box Oparesheni kwa lengo la kuhamasisha wananchi kutambua na kuunga mkono mafanikio ya serikali.

“Katika kila kona ya nchi, watu wanaona kwa macho maendeleo yanayotekelezwa na Rais Samia. Ndiyo maana tunasema, mwaka huu CCM itashinda kwa kishindo katika ngazi zote — Udiwani, Ubunge na Urais,” alisema Sakala.

Katika ziara hiyo, ilizinduliwa pia Ofisi ya UVCCM Kata ya Ndala na kutolewa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji katika Shule ya Msingi Ndala.

Kampeni hiyo ya Mama Full Box Oparesheni yenye kaulimbiu “Kazi na Utu, Tunasonga Mbele” itaendelea katika Kata ya Mjini na Ndembezi siku inayofuata.