Wabunge washauri umri wa mikopo uongeze, wazee wakumbukwe

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 01:25 PM Apr 11 2025
Mbunge wa Jimbo la Nyasa (CCM), Mhandisi Stella Manyanya (kulia) na Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda.
Picha: Mtandao
Mbunge wa Jimbo la Nyasa (CCM), Mhandisi Stella Manyanya (kulia) na Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda.

Wabunge wawili wameibuka na hoja tofauti kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kuongeza kigezo cha umri wa vijana hadi kufikia 50 kuliko 45 ya sasa.

Aidha, mbunge mwingine amependekeza sheria ifanyiwe marekebisho ili wazee nao waingizwe kwneye mikopo hiyo kwa kuwa wanachangamoto za kiuchumi.

Wabunge hao ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa (CCM), Mhandisi Stella Manyanya na Mbunge wa Viti maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda, ambao waliuliza maswali ya nyongeza kwa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk. Festo Dugange, Aprili 11, mwaka huu wakati wa maswali na majibu.

Mbunge Stella ameshauri umri wa vijana kukopeshwa fedha za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmshauri nchini uongezwe hadi kufikia miaka 50 badala ya miaka 45 ya sasa.

Amesema pamoja na kuwa umri uliopangwa wa miaka 45, bado wapo watu ambao wanaingia umri wa miaka 50 wakiwa bado wapo katika hali ya umaskini hivyo serikali haioni kuwa ipo haja kuongeza umri huo hadi miaka 50.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Dk. Festo Dugange, amesema kwasasa utekelezaji wa mikopo hiyo ni kwa mujibu wa sheria, na wataendelea kutekeleza kwa kadri ya matakwa hayo.

Kuhusu hoja ya wazee, Mbunge Sophia ameshauri Bunge lijalo la 13 kufanya marekebisho ya sheria na kanuni zinazosimamia utoaji wa mikopo ya asilimia 10, ili kuongeza wigo wa makundi mengine kunufaika na mpango huo.

Mwakagenda amesema pamoja na kuwa serikali kutunga sheria na kanuni za kutoa mikopo hiyo, lakini mahitaji bado ni makubwa na hasa wazee wamekuwa wengi ambao wanahitaji kuwezeshwa kiuchumi.

“Hatuoni ipo haja kwa bunge lijalo itungwe au kubadilisha hii sheria ili na makundi mengine hasa wanaume wanufaike na utaratibu huu?”amehoji.

Akijibu swali la mbunge huyo, Waziri Dk. Dugange, amesema wamepokea ushauri, lakini kwa sasa wataendelea kuteleza utoaji wa mikopo hiyo kwa mujibu wa sheria.