Watia nia CHADEMA waibuka na hoja tisa kuhusu ‘no reforms no election’

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 05:35 PM Apr 04 2025
Ofisi ya CHADEMA.
Picha: Mtandao
Ofisi ya CHADEMA.

Watia nia 55 wa ubunge kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa mwaka 2025, wakiwakilisha zaidi ya 200 walioonesha nia, akiwemo baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho, wameibuka na hoja tisa kuhusu msimamo wa chama huo wa kutoshiriki uchaguzi endapo hakutakuwa na mageuzi ya kisiasa ('No reforms, no election').

Kupitia waraka walioutuma Aprili 4, 2025 kwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, watia nia hao wameeleza kuwa msimamo huo kwa sasa unakinzana na malengo yake ya awali. Wamedai kuwa haiwezekani kuzuia uchaguzi kwa kuwa nje ya mchakato huo, wakisema hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama kitendo cha jinai.

Kwa mujibu wa waraka huo, njia pekee ya kuzuia uchaguzi usiyo huru ni kushiriki mchakato huo kwa kuingiza wagombea, ambao wanaweza kuhamasisha na kuongoza wananchi kuzuia uchaguzi katika maeneo mahsusi yenye viashiria vya hujuma, badala ya kuwa nje ya mchakato mzima.

Hoja tisa kuu zilizowasilishwa:

1. ✍🏿Mbinu ya Kuzuia Uchaguzi Kutoka Ndani: Waraka umeeleza kuwa kushiriki uchaguzi ni njia bora ya kudhibiti au kuzuia hujuma katika vituo vya uchaguzi kuliko kususia uchaguzi mzima.

2. ✍🏿Asili ya Dhana ya 'No Reforms, No Election': Walibainisha kuwa dhana hiyo ilianza kama kampeni mwaka 2020 baada ya kikao cha Kamati Kuu nchini Kenya (Makueni), na haikuwa na maana ya kuzuia uchaguzi bali ililenga kuhamasisha mageuzi.

3. ✍🏿Muda Umekwenda: Watia nia wameeleza kuwa muda wa utekelezaji wa mkakati madhubuti wa kuzuia uchaguzi umeshapita, huku mchakato wa uchaguzi ukiwa tayari umeanza kupitia zoezi la uandikishaji wapiga kura na mgawanyo wa majimbo.

4. ✍🏿Katiba ya CHADEMA Inasisitiza Ushiriki wa Uchaguzi: Ibara ya 4 ya Katiba ya CHADEMA inaeleza madhumuni ya chama kuwa ni pamoja na kuongoza dola kupitia uchaguzi, hivyo kushiriki uchaguzi ni matakwa ya kikatiba.

5. ✍🏿Haki ya Wanachama Kugombea: Kwa mujibu wa Ibara ya 5.2.2 ya Katiba ya CHADEMA, kila mwanachama ana haki ya kuchaguliwa na kuwakilisha chama katika ngazi mbalimbali, hivyo kuzuia uchaguzi kunaweza kuwa kinyume na haki hiyo.

6. ✍🏿Upweke wa CHADEMA Katika Msimamo: Waraka umeeleza kuwa hadi sasa, hakuna chama kingine cha siasa kinachounga mkono msimamo wa kutoshiriki uchaguzi iwapo reforms hazitapatikana. Vyama vingine vinaendelea kujiandaa kushiriki uchaguzi, huku hata vile vinavyopigania reforms vikiwa bado kwenye maandalizi ya uchaguzi.

7. ✍🏿Msimamo wa Viongozi wa Dini: Viongozi wa dini wameshatoa wito na kuendelea kuhamasisha waumini wao kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura, jambo linaloashiria kuwa jamii inaendelea kujipanga kwa ajili ya uchaguzi.

8. ✍🏿Wadau Wengi Wa Demokrasia Hawajaunga Mkono Kususia Uchaguzi: Uchunguzi wa watia nia unaonyesha kuwa wadau wengi wanaunga mkono hoja ya reforms, lakini si mpango wa kutoshiriki uchaguzi, jambo ambalo linaathiri nguvu ya madai ya msingi.

9. ✍🏿Hatari ya Kukosa Ushiriki Kabisa: Waraka umehitimisha kwa kueleza kuwa iwapo jitihada za kupata reforms zitashindwa na uchaguzi ukaendelea, chama kitapoteza nafasi ya kushiriki uchaguzi kutokana na kutokuwa tayari, hivyo kukosa fursa kabisa ya ushindani.

Waraka huo umeeleza kuwa kwa hali ilivyo sasa, chama kinatakiwa kutathmini upya msimamo wake kuhusu kushiriki uchaguzi ili kulinda nafasi ya kisiasa, kikatiba na kidemokrasia kwa wanachama na taifa kwa ujumla.