WANANCHI wa Mtaa wa Lumumba katika Kata ya Mwembetogwa Halmashauri ya Mji wa Makambako wilayani Njombe, wamekubaliana kulipishana faini ya Sh. 5,000 na sahani dazani moja kwa mtu yeyote ambaye hatahudhuria kwenye msiba.
Maazimio hayo yamefikiwa juzi katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika mtaani hapo kutokana na wananchi wengi kutohudhuria kwenye msiba, hali inayosababisha shughuli mbalimbali hasa uchimbaji kaburi na kupika kutofanyika kwa wakati kutokana na idadi ndogo ya watu wanaohudhuria msibani.
Wakizungumza mara baada ya mkutano huo mmoja wa wananchi hao akiwemo Wiston Kiwanga alisema kutokana na hali hiyo wamelazimika kuweka faini hiyo, kueleza kuwa pia watakuwa na utaratibu wa kuchangia fedha za matatibabu kwa wale ambao ni wagonjwa na hawana uwezo wa kifedha.
“Changamoto mtaani kwetu hawajitokezi kabisa kwenye misiba, ushirikiano ulikuwa ni mdogo sana kwa sababu tunakuwa tupo wachache,” alisema Kiwanga.
Naye, Onesmo Kipela alisema kupitia makubaliano hayo yatasaidia kila mmoja kuwajibika.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mwembetogwa ambaye anakaimu Mtaa wa Lumumba, Eden Mbogela alisema hali ya wananchi kutohudhuria msibani inasababishwa na kukosekana kwa uelewa wa umuhimu wa kushiriki kwenye shughuli za kijamii.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Lumumba, Mwalimu Rashid Martin alisema licha ya changamoto ya wananchi kutohudhuria msibani pia kuna tatizo la wananchi hao hasa wapangaji kutotambuana wao kwa wao licha ya kuishi nyumba moja na kutojua namba za nyumba wanazoishi.
Diwani wa Kata ya Mwembetogwa, Odo Chaula aliwataka wananchi kushiriki kwenye masuala ya kijamii na serikali ili kudumisha umoja na amani, huku wakiwataka kujiandaa na uchaguzi wa mkuu utakaofanyika mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED