Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita, amesema chama hicho kinapinga vikali unyonyaji na uonevu wanaofanyiwa wafanyakazi wa viwandani, wachimbaji wadogo, na wafanyakazi wa majumbani kwa kulipwa ujira mdogo usioendana na kazi wanazozifanya.
Akizungumza leo Aprili 4, 2025 katika Mjadala wa Kitaifa wa Ajira uliofanyika Makao Makuu ya ACT Wazalendo Magomeni, Mchinjita amesema:
"Tunaona wafanyakazi wakifanya kazi zaidi ya saa 12 kwa malipo ya chini ya Shilingi 200,000 kwa mwezi. Wachimbaji wadogo wanadhulumiwa na makampuni makubwa bila msaada wa serikali. Wafanyakazi wa majumbani wanafanyishwa kazi katika mazingira ya kinyama. Huu ni mfumo wa unyonyaji ambao ACT Wazalendo inaupinga kwa nguvu zote," amesisitiza.
Mjadala huo uliwaleta pamoja Mawaziri Vivuli wa ACT Wazalendo, wanafunzi wa vyuo vikuu, pamoja na viongozi wa Umoja wa Vijana Wasiokuwa na Ajira (UYAM), kwa lengo la kuchambua hali ya ajira nchini na kutafuta njia za maboresho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana wa ACT Wazalendo, Abdul Nondo, ameeleza kusikitishwa na hali ngumu inayowakumba vijana katika sekta isiyo rasmi, hasa wamachinga wanaohamishwa kila mara bila utaratibu.
"Vijana katika sekta isiyo rasmi ni zaidi ya asilimia 80. Kila siku wanakimbizwa, hawana bima ya afya wala pensheni. Ndio maana nasema vijana tuungane na tupaze sauti dhidi ya ukosefu wa ajira na mustakabali wetu," amesema Nondo.
Chama hicho kimesisitiza kuwa kipo tayari kupaza sauti ya walio wengi, hasa vijana na wafanyakazi, kwa lengo la kujenga taifa lenye usawa na haki za kiuchumi kwa wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED