Dk. Mhina: Watumishi LITA zingatieni maadili ya utumishi wa umma
By
Paul Mabeja
,
Nipashe
Published at 06:54 PM Apr 04 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Mhina
Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Mhina, amewataka watumishi wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kuongeza ufanisi na tija kazini.
Akizungumza leo Aprili 4, 2025, jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Riziki Shemdoe, wakati wa kikao cha utoaji taarifa za mkutano wa 12 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa LITA, Dk. Mhina amesema baadhi ya watumishi wamekuwa wakishindwa kufuata kanuni na sheria za utumishi wa umma kutokana na uzembe, hali inayochangia kuzorota kwa utendaji.
"Tufanye kazi kwa bidii na kwa uaminifu tukizingatia misingi mikuu ya uadilifu, uwajibikaji na utiifu. Tusitumie taarifa za Serikali visivyo au bila idhini ya utawala," amesisitiza Dk. Mhina.
Ameitaka Menejimenti ya LITA kuhakikisha inawajengea uwezo watumishi wake ili waendelee kutoa huduma bora zenye kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma.
Mtendaji Mkuu wa LITA, Dk. Pius Mwambene.Vilevile, amewapongeza kwa mpangilio mzuri wa kampasi zao ambazo zimekuwa zikitoa fursa za maendeleo kwa wafugaji, lakini pia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu na ushirikishwaji wa jamii katika kutoa mafunzo ya mifugo.
Aidha, Dk. Mhina ameipongeza Kamati ya Wajumbe wa Baraza Kuu la LITA kwa juhudi za kuanzisha vyuo katika maeneo mbalimbali nchini na amehimiza kuendelea kubuni miradi mipya yenye tija ili kusaidia maboresho ya taasisi kwa miaka ijayo.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa LITA, Dk. Pius Mwambene, amesema wamepokea kwa uzito nasaha zilizotolewa na mgeni rasmi na watahakikisha wanafanya kazi kwa ushirikiano katika kutekeleza mipango ya mwaka ujao wa fedha.
"Tutaendelea kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kutekeleza majukumu tuliyopewa na Serikali kwa uwajibikaji mkubwa ili kuleta matokeo chanya kwa taasisi na Taifa kwa ujumla," amesema Dk. Mwambene. 1