Mvutano wa kisiasa ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) umeibuka kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii, ukihusisha makundi mawili yenye mitazamo tofauti kuhusu ushiriki wa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mzozo huo unahusisha kundi la watia nia 55 (maarufu kama G55) waliomwandikia Katibu Mkuu wa chama, John Mnyika, waraka wa wazi wakitoa hoja tisa za kupinga msimamo wa chama wa kutoshiriki uchaguzi bila kufanyika kwa mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi, msimamo unaojulikana kama “No Reforms, No Election.”
Kundi hilo limekuwa likituhumiwa na baadhi ya wanachama na wafuasi wa CHADEMA kuwa wamelipwa ili kuvuruga umoja wa chama, huku wakidai kuwa nia yao ni kuchochea umwagaji wa damu.
Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema, ameandika ujumbe mrefu katika ukurasa wake wa X kujibu tuhuma hizo, huku akiwataka wanaopinga waraka huo kuheshimu mitazamo tofauti.
“Panic mood activated! Hamjazoea kusikia maoni tofauti na yenu. Mnataka kila mtu aamini kama ninyi — huo siyo uhuru wala demokrasia,” ameandika Mrema.
Akiendelea kujibu tuhuma kuwa G55 wamelipwa na kwamba wanataka uchaguzi ufanyike kwa nguvu:
“Kuingia kwenye uchaguzi si kumwaga damu. Kuzuia uchaguzi ndiyo suluhisho la amani? Acheni propaganda.”
Mrema pia amekanusha madai kuwa waandishi wa waraka huo wanafadhiliwa na vyombo vya usalama, huku akieleza kuwa wapo wazi na wanajulikana tofauti na wanaotoa tuhuma wakiwa nje ya nchi.
“Tunalipwa na usalama? Hivi kati yetu sisi na ninyi mnaoishi Nairobi bila kujulikana mnafanya kazi gani, nani anaonekanika zaidi?”
Amesema wanaounga mkono msimamo wa kususia uchaguzi wanaifanya CHADEMA iingie kwenye mtego wa kuiwezesha CCM kupita bila kupingwa, jambo ambalo ni hatari kwa demokrasia.
“Mnadhani kuzuia uchaguzi ni njia sahihi? Hapo ndipo CCM inapita bila bugudha. Nani anamsaliti mwenzie?”
Mrema ambaye ametangaza nia ya kugombea ubunge Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, ameeleza kuwa watu walioko nje ya nchi ndio wanaochochea mgawanyiko kwa kutaka uchaguzi usifanyike huku wao wakiwa salama.
“Wanaotaka damu ni ninyi mnaowataka Watanzania wakate uchaguzi huku ninyi mkiwa nje — salama! Kama mna msimamo, rudi mstari wa mbele.”
Amehitimisha ujumbe wake kwa kusema kuwa huu si wakati wa kimya, bali wa kusema ukweli, hata kama unauma.
“Ukimya sasa basi! Najua hamkuzoea kusikia ukweli mchungu. Lakini huu ni wakati wa kuambiwa!”
Mvutano huu umewaacha baadhi ya wanachama wa CHADEMA wakiwa njia panda, huku wakihoji iwapo mgawanyiko huu unaweza kuathiri maandalizi ya uchaguzi na mustakabali wa chama hicho kuelekea 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED