Waliodai kubadilishiwa mtoto waangua kilio baada ya majibu ya DNA

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 07:56 AM Apr 04 2025

Waliodai kubadilishiwa mtoto waangua kilio baada ya majibu ya DNA
Picha: Mpigapicha Wetu
Waliodai kubadilishiwa mtoto waangua kilio baada ya majibu ya DNA

Hatimaye majibu ya vinasaba (DNA) ya watoto watatu waliozaliwa Machi 24, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha (Mount Meru) yametolewa, huku Neema Kilugala, mkazi wa mtaa wa Ndaravoi, Kata ya Daraja Mbili jijini Arusha, akiangua kilio baada ya kutoridhishwa na matokeo hayo.

Neema ambaye alijifungua kwa upasuaji katika hospitali hiyo, alidai kuwa alibadilishiwa mtoto na hakuwahi kuridhika na mtoto aliyekabidhiwa, akisema mtoto wake alizaliwa akiwa mzima wa afya na mwenye uzito wa zaidi ya kilo tatu.

Akizungumza kwa uchungu nje ya Kituo Kikuu cha Polisi mkoani Arusha Aprili 3, 2025, Neema alisema anaamini kuwa mtoto wake yupo hai na kuna mwanamke mwingine aliyepewa mtoto wake kwa bahati mbaya au makusudi.

Mama mzazi wa Neema naye alilia kwa uchungu, akiitaka serikali irejee upya vipimo vya DNA kwa watoto wote watatu, kwa kuwa mtoto ambaye inadaiwa ni wa binti yake (Neema) na tayari ameshafariki, si wake kwa mujibu wa maumbile na hisia zao za kizazi.

Kutokana na utata huo, serikali iliamuru kufanyika kwa vipimo vya DNA kwa wanawake wote waliowajifungua watoto siku hiyo pamoja na watoto wao, ili kupata ukweli wa jambo hilo.

Kwa mujibu wa Afisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. George Daniel, ambaye yupo jijini Arusha kupitia kampeni ya "Samia Legal Aid", alisema walipokea wito kutoka Polisi kwa ajili ya kushiriki katika kusikiliza majibu ya vinasaba hivyo.

“Katika matokeo haya, ambapo wazazi wote watatu walikuwepo, vipimo vimeonyesha kwa asilimia zaidi ya 99 kuwa mtoto anayelalamikiwa na Neema kuwa si wake, ndiye mtoto wake halisi kwa mujibu wa vinasaba,” alisema Bw. Daniel.

Aliongeza kuwa, iwapo Neema bado anahitaji msaada wa kisheria, ofisi yao iko tayari kumsaidia kupitia kampeni ya Samia Legal Aid ambayo inalenga kuwasaidia wananchi wanyonge kupata haki zao.

Diwani wa Kata ya Daraja Mbili aliyefika kituoni hapo pamoja na familia ya Neema alisema kuwa wataitisha kikao cha pamoja kujadiliana hatua za kuchukua kufuatia matokeo hayo.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) alitoa wito kwa wauguzi nchini kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, akibainisha kuwa chama hicho kitaendelea kufuatilia kwa karibu utendaji kazi wa wauguzi kuhakikisha haki na uadilifu vinaendelea kutawala katika huduma za afya.