Wizara yataja vikwazo ufugaji nguruwe

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 02:12 PM Sep 11 2025
Katibu Mkuu wa  Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena
Picha: Mtandao
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema miongoni mwa vikwazo kwa wafugaji wa nguruwe, ni pamoja na ugonjwa wa homa ya nguruwe, gharama za chakula na kukosekana kwa masoko ndani na nje ya nchi.

Agnes, ameyasema hayo leo Septemba 11, 2025 katika kongamano maalumu lililowakutanisha wafugaji wa nguruwe na wadau wa sekta hiyo, ndani na nje ya nchi.

Amesema sekta ya nguruwe kwa sasa inakua kwa kasi na imechangia vijana wengi kupata ajira na kwamba idadi ya wafugaji kwa Afrika inazidi milioni nne.

Amesema kongamano hilo linahitajikita zaidi katika kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, sambamba na kuweka mikakati ya kuondoa ugonjwa huo alioutaja kama ni kikwazo kikubw kwa wafugaji.

Aidha amesema mkutano huo utawasaidia wafugaji nchini kujenga ukaribu na wale wa nje ya nchi pamoja na kubadilishana uzoefu utakao wasaidia kuboresha ufugaji wao. 

"Serikali kazi yetu kutoa huduma, tafiti, tiba, na kuwawezesha wakulima na wengine kwaajili kupata masoko" amesema 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafugaji wa Nguruwe Tanzania, Doreen Maro, amesema sekta ya ufugaji wa wanyama hao inakua kwa kasi, kutokama na upatikanaji mbegu nzuri ambazo ni matokeo ya jitihada za jumuiya hiyo. 

Amewataka watu mbalimbali, ikiwamo wastaafu na vijana kujitosa katika ufugaji wa nguruwe akisisitiza unalipa na ni biashara nzuri.

Mfugaji Ziaka Lameki, ameshukuru kongamano hilo kujadili kuhusu namna ya kukabili changamoto zinazoikabili sekta hiyo, akitamba sasa ataweza kufuga kisasa na kupata matokeo makubwa.