Mahakama Kuu yamrejesha Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 05:48 PM Sep 11 2025
Mahakama Kuu yamrejesha Mpina kwenye kinyang’anyiro cha urais

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu ya Dodoma, imemrejesha Luhaga Mpina kwenye mbio za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.


Uamuzi huo umetolewa leo na Mahakama hiyo wakati wa kusoma hukumu ya kesi iliyohusu pingamizi la uteuzi wa Mpina. Katika maamuzi yake, Mahakama imetamka wazi kuwa mgombea huyo ana haki ya kikatiba ya kuwasilisha fomu za uteuzi kama walivyofanya wagombea wengine.

Aidha, Mahakama Kuu imeelekeza Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) kufungua mlango wa kurejesha fomu, ili Mpina aweze kuwasilisha nyaraka zake za uteuzi wa kugombea urais kwa mujibu wa sheria na taratibu za uchaguzi.

Katika maelezo yake, Mahakama imesisitiza kuwa kitendo cha INEC kumzuia Mpina kurejesha fomu za uteuzi kilikuwa kinyume cha Katiba, hivyo mchakato huo unatakiwa kuendelea kutoka pale ulipoishia. Pia, imetamka bayana kuwa Tume hiyo ni huru kwa mujibu wa jina na hadhi yake, hivyo haipaswi kupokea maelekezo yoyote kutoka serikalini.

Kuhusu ombi la fidia lililotolewa na mleta maombi wa pili, Mpina, Mahakama imesema kutokana na mazingira ya kesi hiyo, haiwezi kutoa maamuzi juu ya suala hilo.

Shauri hilo lilisikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Abdi Kagomba, ambapo msingi wa kesi ulikuwa ni pingamizi dhidi ya uteuzi wa Mpina kama mgombea urais kupitia ACT-Wazalendo. Pingamizi hilo liliibuliwa na kada wa chama hicho, Monalisa Ndala, aliyedai kuwa chama kilikiuka Katiba, Sheria na Kanuni za uchaguzi wakati wa kumteua Mpina kuwa mgombea Agosti 27, mwaka huu.

Hata hivyo, viongozi wa juu wa chama hicho waliwahi kubainisha kuwa hakuna taratibu zilizokiukwa katika kumpitisha Mpina kuwania nafasi hiyo, hali iliyozua sintofahamu ndani ya chama kabla ya shauri hilo kufikishwa mahakamani.