Ukarabati MV Liemba wafikia asilimia 32-TASHICO

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:17 PM Sep 11 2025
Ukarabati MV Liemba wafikia asilimia 32-TASHICO
Picha: Mpigapicha Wetu
Ukarabati MV Liemba wafikia asilimia 32-TASHICO

Ukarabati wa meli kongwe zaidi ya abiria Duniani, MV Liemba wenye lengo la kuirudisha kama ilivyokuwa wakati ikianza kazi mwaka 1915 unaendelea vyema ambapo hadi kufikia tarehe 9 Septemba 2025 mradi ulikuwa umefikia asilimia 32 ya utekelezaji.

Akizungumza muda mfupi mara baada ya kutembelea ukarabati wa meli hiyo kongwe mkoani Kigoma, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO) Eric B. Hamissi alisema kuwa maendeleo ya ukarabati wa meli hiyo ya kihistoria ambayo ni tegemeo muhimu kwa jamii iliyopo pembezoni mwa Ziwa Tanganyika unaendelea vizuri ambapo kwa saa umekamilika kwa asilimia 32. 

"Niko hapa kuangalia maendeleo ya ukarabati wa meli ya MV Liemba ambayo sasa imekamilika kwa asilimia 32 na ukarabati huu mkubwa ni kuhakikisha inaendelea kufaya kazi kwa ufanisi mkubwa katika Ziwa Tanganyika," alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa TASHICO amesema kuwa MV Liemba ni tegemeo muhimu kwa wakazi walipo jirani na Ziwa Tanganyika ambapo ukarabati wake utaboresha hali zao kiuchumi pamoja na huduma za usafiri kwa ujumla.

Meli ya MV Liemba iliyojengwa na Wajerumani kutoka enzi ya vita ya kwanza ya Dunia na kuchukuliwa kuwa meli ya mwisho ya Jeshi la Wanamaji wa Ujerumani inakarabatiwa kwa gharama ya shilingi bilioni. 

Kampuni ya Croatia ya M/S Brodosplit JSC, kwa kushirikiana na Dar es Salaam Merchant Group (DMG), ndiyo walipewa kandarasi ya kufanya ukarabati wa meli hiyo ya kihistoria.

Hata hivyo, Wananchi waishio kandokando ya Ziwa Tanganyika hasa mkoani Kigoma wamefurahishwa na ukarabati wa meli hiyo ya kihistoria ya MV Liemba wakisema ukarabati huo utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya usafiri wa majini katika Ziwa Tanganyika hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi kwa jamii zinazoishi mwambao wa ziwa hilo.

"Tunafurahia kuona ukarabati wa meli hii ambao umedhamiria kuboresha huduma za usafiri na kukuza uchumi wetu ukiendelea vyema," Juma Ramadhani mfanyabiashara wa Kigoma alisema.

Mkazi mwingine wa Kigoma, Joyce Charles ametoa shukrani kwa serikali katika ukarabati wa meli hiyo kongwe, akisema kwamba baada ya kukamilika kwa meli hiyo wataweza kusafirisha bidhaa zao na wao wenyewe kwa haraka na rahisi hivyo kuinua uchumi wa nchi na wakazi wa pembezoni mwa Ziwa Tanganyika.

Meli ya MV Liemba inauwezo wa kubeba jumla ya tani 200 za mizigo na abiria 600. Meli hii ya kihistoria iliyojengwa mwaka 1913 na kuzinduliwa kwenye Ziwa Tanganyika mwaka 1915, imekuwa ikifanya kazi kwa zaidi ya karne moja, ikitumika kama kiungo muhimu cha usafiri kati ya Tanzania na Zambia. Pamoja na ukarabati wake, meli ya MV Liemba inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa mkoa wa Kigoma na jamii inayozunguza ziwa hilo lenye ukubwa wa pili nchini.