Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, ametangaza neema kwa wakulima wa tumbaku kuwa serikali inakwenda kulibeba zao hilo kwa kutafuta masoko bora zaidi.
Pia ameonya ukataji wa miti, akiagiza wakulima hao kujikita katika teknolojia ya kisasa kulikausha zao hilo.
Alitoa ahadi hiyo leo Septemba 11, 2025, katika mikutano ya kampeni za urais aliyofanya wilayani Uyui, Utambo na Kaliua, mkoani Tabora, akiendelea kunadi sera na ilani za chama hicho na kuomba kura kwa wananchi.
Akizungumza na wananchi wa Uyui, Samia alisema serikali imefanikiwa kuongeza kampuni za kununua tumbaku, ili kupanua wigo wa masoko kwa wakulima hao.
“Nimeambiwa kuna wakulima wa tumbaku wenye madai yao ya siku nyingi mtalipwa,” ameahidi.
Akizungumza katika mkutano mwingine Urambo, Dk. Samia amesema mwaka 2021/22, Bashe akiwa Naibu Waziri Kilimo, uzalishaji tumbaku ulikuwa tani 11,208 lakini kwa sasa akiwa Waziri kamili, umefikia tani 20,492.
“Wakati ule tumbaku ilinunuliwa kwa kuchambuliwa daraja la kwanza, la pili, la tatu na nyingine haikuchukuliwa kwa kuonekana haifai.
“Bashe amejitahidi kutafuta kampuni wanachukua tumbaku yote hakuna inayoachwa. Amefungua kiwanda pale Morogoro, tumbaku ikizalishwa inakwenda pale kuongezwa thamani na kusafirishwa nje ya nchi,” amesema.
Mgombea huyo wa urais amesema mwaka 2021/22 wakulima walipokea Dola milioni 11 na mwaka 2024/25 Dola milioni 50 ambazo ziliingia hapa ndani.
“Sishangai kuona maendeleo ya makazi Urambo nyumba zimebadilika. Bashe amejitahidi kupandisha bei za tumbaku. Tulipoingia bei ilikuwa Dola moja kwa tani kwa sasa ni Dola 2.5 kwa tani 2.5, imepanda kwa asilimia 120.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED