Zanzibar yazindua Wiki ya Afya, lengo kukuza Utalii wa Tiba

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 06:50 PM Apr 11 2025
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.
Picha: Imani Nathaniel
Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui.

Waziri wa Afya wa Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, kwa kushirikiana na Kamati ya Afya ya Mkoa wa Dar es Salaam, wamezindua rasmi Wiki ya Afya ya Zanzibar itakayofanyika mwezi Mei mwaka huu visiwani humo.

Akizungumza leo Aprili 11, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Waziri Mazrui amesema lengo la wiki hiyo ni kuunganisha wataalamu wa sekta ya afya na wananchi kwa ujumla, sambamba na kuchochea utalii wa tiba ambao utawanufaisha watu wengi kupitia huduma mbalimbali zitakazotolewa.

"Huduma hizi zitaongeza uelewa wa afya na kinga kwa wagonjwa wa aina mbalimbali, huku tukikuza utalii wa tiba kwa wale wanaokuja kutoka nje ya nchi kwa ajili ya huduma kama kujifukiza na nyinginezo za kiafya," amesema Waziri Mazrui.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Musa Mohamed Musa, amesema wamejipanga kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya Zanzibar ili kuimarisha utalii wa afya, ambao ni sehemu muhimu ya maendeleo ya sekta hiyo.

1

"Utalii wa afya una nafasi kubwa ya kuunganisha sekta binafsi na za umma, hivyo kuongeza mapato ya taifa na kutoa ajira kwa vijana," ameongeza Dk. Musa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar,Mangere Mzee Miraji, amesema uzinduzi wa wiki hiyo ni fursa kwa Watanzania kuibua njia mbadala za mapato kupitia utalii wa ndani, sambamba na kuboresha huduma za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

"Kwa kushirikiana na wadau wa afya kutoka Dar es Salaam, tunaamini kuwa mahusiano haya yatasaidia kuboresha huduma na kuwafikia makundi yenye changamoto mbalimbali za kiafya," amesema Miraji.

Wiki ya Afya ya Zanzibar inatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutoa huduma za afya, elimu ya kinga, pamoja na kutangaza vivutio vya utalii wa tiba kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.