Kanuni kutaka wacheze wageni nane tu haikubaliki

Nipashe
Published at 07:45 AM Jul 15 2024
 Ligi Kuu Tanzania Bara.
Picha:Mtandao
Ligi Kuu Tanzania Bara.

KUNA taarifa kuwa moja kati ya mapendekezo ya kanuni zitakazoendesha Ligi Kuu msimu ujao, ni kuzuia wachezaji wote 12 wa kigeni kutocheza katika mechi moja, badala yake wadau wanapendekeza wawe wanane tu.

Katika kumbukumbu zetu, hii si kanuni mpya kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, kuna wakati ilishakuwapo, lakini ikalalamikiwa sana na wadau wa soka, wakiwamo makocha mbalimbali waliokuwa wakifundisha klabu nchini hasa wa Simba na Yanga.

Tunajua kuna mapendekezo ya kanuni bora kabisa ambazo zitaufanya mpira wetu kuendelea kupanda na kupendwa Afrika, lakini si hii ya kutaka wachezaji wanane wa kigeni ndiyo wacheze kwenye mechi moja.

Nadhani bado kuna wadau wa soka hawajatambua ni kwa nini soka la Tanzania kwa sasa limekuwa gumzo, limetokea kupenda Afrika, kiasi cha kuwa namba sita.

Haijafika hapo kwa bahati mbaya, ni kwamba imeruhusu wachezaji wa kigeni wacheze kwa kujinafasi, na hiyo imezifanya timu za Simba na Yanga kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa mfululizo kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya soka la Tanzania.

Huwezi kuelezea mafanikio ya Simba kwa miaka mitano mfululizo au miwili ya Yanga bila kuwataja wachezaji wa kigeni kina Meddie Kagere, Haruna Niyonzima, Clatous Chama, Emmanuel Okwi, James Kotei, Sadio Kanoute, Djigui Diarra, Djuma Shaaban, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli, Fiston Mayele, Stephane Aziz Ki, na wengineo wengi waliokuwa wakiunda vikosi vya timu hizo.

Ukiwaondoa hao, sidhani kama Simba na Yanga zingeweza kufika hapo, kwani huko nyuma wakati zikitumia wazawa wengi, hata kuingia makundi tu Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ilikuwa mtihani.

Ndiyo msimu uliomalizika Yanga wakiingia makundi Ligi ya Mabingwa mara ya kwanza tangu 1998, na Simba iliingia 2017/18, mara ya kwanza baada ya 2003.

Uwapo wa wachezaji wengi wa kigeni ndiyo umefanya hivi Tanzania iwe na nafasi nne za uwakilishi, lakini pia hata viongozi wa pande zote mbili wakiwa na uwezo wa kusimama mbele ya watu kusema wanataka ubingwa wa Afrika, wachezaji hao wamesabisha hata Timu ya Taifa ya Tanzania kwa sasa kuwa imara na kutoziogopa hata za mataifa ya nje yenye majina makubwa.

Hii ni kwa sababu wachezaji wengi wanacheza nao kwenye ligi au wapo timu moja. Hivyo kuwapunguza tunatengeneza nafasi nne za wachezaji ambao wana uafadhali na si kiwango cha soka, hivyo hata wakichanguliwa Stars wanakwenda kwa sababu wanacheza mara kwa mara kwenye timu na wale si viwango vyao.

Tunaomba Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) na Bodi ya Ligi nchini (TPLB), kutupilia mbali mapendekezo hayo kwani yataleta athari kubwa katika soka letu. Tunataka Mtanzania akipata namba, basi awe amewazidi viwango wageni ama analingana nao na si kwa kubebwa na kanuni, hapo ndipo tunatapowapata wachezaji wazuri kikosi cha Taifa Stars.

Kwa miaka hii michache ambapo hakuna kanuni za ajabu za kuwazuia wageni, wakiwa 12 na kocha ana uwezo wa kuwachezesha wote, ndipo tumeiona Stars bora zaidi, yenye wachezaji waliokomaa na kupambana kutokana na kukomazwa na wageni hao hao.

Kutowawekea kanuni ya upendeleo, kumewafanya wachezaji kwa ubora kama Ibrahim Hamad 'Bacca', Mudathir Yahaya, Dickson Job, Clement Mzize, Nickson Kibabage, kupigania namba na kuwaweka benchi wageni upande wa Yanga, Mohamed Hussein 'Tshabalala', Shomari Kapombe, Mzamiru Yassin, hata Ladack Chasambi, na Edwin Balua kuonyesha makali yao wakiwa na timu ya Simba, huku kule Azam mchezaji Feisal Salum na Yahaya Zayid hata hawahitaji kanuni hiyo ili kupata nafasi Stars.