Ni wakati wa wazawa kupambania namba

Nipashe
Published at 02:18 PM Jul 08 2024
Ni wakati wa wachezaji wazawa kupambania namba.
Picha: Maktaba
Ni wakati wa wachezaji wazawa kupambania namba.

WAKATI klabu za Ligi Kuu zipo katika harakati za kufanya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano, tunaona idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni wakisajiliwa na timu hata zile ambazo huko nyuma zilikuwa hazifanyi hivyo, sasa nazo zimeamua kushusha wachezaji kutoka nje ya nchi.

Klabu kama KMC na hata Prisons ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa zikiamini wazawa, zimeanza kuleta wachezaji kutoka nje, huku ‘Wajelajela’ hao wao wakianza hivyo tangu msimu uliopita.

Siku kadhaa nyuma nilimsikia kiongozi mmoja wa Mashujaa FC, naye akitamani kikosi hicho kiwe na wachezaji wa kigeni, ambapo alisema wanaweza kuomba kibali kwa ajili hiyo, ingawa hatuna uhakika kama wataruhusiwa.

Kwa jinsi tunavyoona ni kwamba huenda msimu ujao klabu 14 zinaweza kuwa na wachezaji wengi wa kigeni, kasoro Mashujaa FC, na JKT Tanzania tu, na si kwa sababu hazitaki, bali ni sababu za kiusalama kwani zinamilikiwa na majeshi yetu ya Ulinzi na Usalama.

Klabu kama Simba, Yanga na Azam tuna uhakika zitakuwa na wachezaji 12 wanaoruhusiwa kikanuni, lakini pia Singida Black Stars na Tabora United, inawezekana ikawa hivyo hivyo.

Zilizobaki zinaweza kuwa na angalau wasiopungua watano kushuka chini. Pamoja na idadi hiyo, bado kimahesabu wachezaji wa Kitanzania watakuwa wengi kuliko wageni.

Ambacho tunashauri kwa wachezaji wa Kitanzania ni kuchukua changamoto hiyo kuwa chanya kwao kuliko hasi.

Huu ni wakati wa kufanya mazoezi kwa bidii ili kuwashawishi makocha wawapange kwa jambo ambalo litatoa nafasi kwao kuitwa kwenye Timu ya Taifa, Taifa Stars.

Hakuna kocha yeyote anayeweza kupanga kikosi chake kwa sababu ya upendeleo wa wageni au wenyeji, bali ni kwa jinsi mchezaji atakavyoonekana anachokifanya mazoezini.

Kocha hupanga yule ambaye atampa matokeo, na yupo tayari kupambania timu kwa wakati huo, haijalishi ni mgeni ama mzawa.

Kwa bahati mbaya sana baadhi ya wachezaji wa Kitanzania hawajitambui na wana tabia ya kubweteka na mafanikio kiduchu na si wapambanaji. Wengi wanapenda tu kusaidiwa na kubebwa na kanuni, na si uwezo wao uwanjani.

Baadhi yao wanaridhika na mishahara mikubwa wanayoipata haswa wanapokuwa kwenye vikosi vya Simba, Yanga na Azam, magari na starehe za muda mfupi, kiasi cha kushindwa kuonyesha viwango walivyokuwa navyo huko walikotoka kabla hawajafika timu hizo.

Matokeo yake msimu mmoja baadaye wanatokewa kwa mkopo na kuishia huko kwani imekuwa mara chache sana kurudishwa tena baada ya kutolewa kwa mkopo.

Mfano msimu uliopita kwenye kikosi cha Simba, wenye uhakika wa kupata namba walikuwa ni wanne tu, Shomari Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Kibu Denisi na Mzamiru Yassin, namba zingine zote zilitawaliwa na wageni.

Kwa sasa Simba ina makocha wapya ambao hawamfahamu yeyote, hivyo ni wakati wao kuchangamka, kumuonyesha walichonacho, pamoja na bidii, kujituma ili kumshawishi kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.

Inaonekana si wachezaji wengi wa Kitanzania waliotapakaa ulimwenguni kwa ajili ya kusaka malisho kama nchi za wenzetu, na hata baadhi yao waliokuwa huko, msimu huu wamerejea nchini, kama Abdulrazack Hamza aliyerejea kutoka Afrika Kusini alipokuwa akiichezea Klabu ya Super Sports na Oscar Paul aliyejiunga na KMC, akitokea Kakamega Home Boys, hivyo kilichobaki ili kutengeneza kikosi bora zaidi cha Stars ni kung’ang’ana kufanya vizuri kwenye mazoezi, kujituma na kufuata maelelezo ya mwalimu ili kupata namba.

Tuna uhakika Mtanzania yeyote ambaye atakuwa kwenye kikosi cha kwanza katika timu yenye wachezaji wengi wa kigeni, anafaa kabisa kuichezea Taifa Stars, hivyo ni wakati sasa kwao kupambana.