Soko limepatikana ni wakati wa kuchangamkia kilimo cha parachichi

Nipashe
Published at 10:09 AM Jul 09 2024
Parachichi.
Picha: Mtandao
Parachichi.

MATUNDA ya parachichi yametokea kupendwa na soko lake ni kubwa duniani kutokana na faida zinazopatikana kutoka kwenye tunda hilo.

Kwa Tanzania tumebahatika kuwa na mikoa ambayo zao hilo linastawi vizuri na utafiti unaonesha kuwa parachichi kutoka nchini kwetu lina ubora kulinganisha na nchi zingine zinazozalisha tunda hilo.

Mwishoni mwa wiki Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwahimiza wananchi wa mkoa wa Iringa na Watanzania kwa ujumla waingie kwenye kilimo cha matunda hayo kwa kuwa zao hilo linachochea ukuaji wa uchumi.

Serikali imefanya juhudi katika kipindi cha miaka mitatu, kutafuta masoko kwa ajili ya maparachichi yanayozalishwa nchini badala ya kutegemea nchi jirani pekee.

Nchi ambazo kuna soko la uhakika ni China na India kutokana na thamani kubwa na ubora wa hali ya juu ya maparachichi yanayozalishwa Tanzania ukilinganisha na kutoka nchi nyingine.

Watanzania wametakiwa kuingia kwenye mpango wa kuzalisha miche ya zao hilo ili kuongeza idadi ya uzalishaji wa maparachichi. Hiyo ni kutokana na ubora mkubwa. Na hii ni baada ya kupima udongo nchini kote na kubaini kuwa Tanzania ina maeneo yenye udongo unaofaa kwa kilimo hicho.

Pamoja na kuhimiza kilimo hicho, pia suala la miundombinu ya barabara lazima lizingatiwe ili matunda hayo yatakapofikia msimu wa mavumo yasiozee mashambani kwa kushindwa kusafirishwa kwasababu ya ubovu wa barabara.

Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) pamoja na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), wana jukumu kubwa la kuhakikisha miundombinu ya barabara inapitika vizuri.

Tanzania ina Baraka ya kupata ardhi nzuri ya mazao na mavuno mengi, lakini tatizo kubwa ni usafirishaji wa mazao kwenda sokoni kutokana na barabara mbovu ambazo wakati wa mvua ndio hali huwa mbaya zaidi. Tatizo hilo husababisha wakulima kupata hasara kutokana na mazao mengi kuozea kwenye maghala au mashambani kwa ugumu wa kusafirishwa.

Hivyo ni muhimu wakati wananchi wanahamasishwa kilimo hicho, iendane sambamba na kasi ya utengenezaji wa miundombinu ya kusafirisha mazao hayo.

Pia, wananchi wapewe elimu ya kutokubali wafanyabiashara wanaokwenda kuwarubuni kwa kununua mazao yakiwa hayajakomaa na kuuza kwa bei ya chini. 

Ni habari njema kutoka kwa Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, kuwa serikali imeshasaini mkataba na kampuni ya Afac Engineering ambayo itajenga kiwanda cha kusindika maparachichi katika eneo la Nyololo ambapo katika awamu ya kwanza, Sh. bilioni 3.4 zitatumika.

“Wana-Mufindi ni watu wanaolima sana. Mbunge wenu amesimamia ahadi ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kujenga kiwanda cha kusindika maparachichi. Mkataba ulisainiwa na kabla ya Ijumaa ijayo, tutamkabidhi eneo mkandarasi ili aanze kazi.”

Kujengwa kwa viwanda vya kuchakata matunda ni njia nzuri ya kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa nchini badala ya kuuza ghafi.

Wanunuzi wa bidhaa zetu ghafi huenda kuzichakata na kuja kuziua nchini kwetu kwa bei za juu, hali inayokosa mapato nchi.

Ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao utasaidia pia, kuokoa yanayooza shambani kwa kuongezewa thamani.