Wawakilishi wa Tanzania jiandaeni vizuri CAF

Nipashe
Published at 07:30 AM Jul 13 2024
Nembo ya Shirikisho la soka Afrika (CAF).
Picha: Mtandao
Nembo ya Shirikisho la soka Afrika (CAF).

SHIRIKISHO la soka Afrika (CAF) lilichezesha droo ya timu zitakazokutana kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho ambapo wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano hiyo tayari wamewafahamu wapinzani wao.

Kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, mabingwa wa soka Tanzania, Yanga wenyewe wataumana na Mabingwa wa Burundi, Vital'O Club huku Azam FC ikipangwa kucheza na APR ya Rwanda ambapo Yanga wataanzia ugenini huku Azam wakianzia nyumbani kati ya Agosti 16 na 18.

Katika droo hiyo iliyochezeshwa Makao Makuu ya CAF, Cairo, Misri, timu zote za Tanzania zitaanzia hatua ya awali isipokuwa Simba inayoshiriki Kombe la Shirikisho itaanzia hatua ya kwanza kwa kusubiri mshindi kwenye mchezo kati ya Uhamiaji FC ya Zanzibar na mwakilishi kutoka Libya ambaye bado hajapatikana.

Katika kombe hilo, Coastal Union yenyewe itacheza na FC Bravos do Maquis ya Angola katika hatua ya awali.

Mwakilishi mwingine wa Zanzibar michuano hiyo, JKU inayoshiriki Ligi ya mabingwa yenyewe imepangwa kucheza na Pyramids ya Misri na mshindi katika mchezo huo atacheza na mshindi kati ya Azam FC na APR.

Michezo ya marudiano imepangwa kuchezwa kati ya Agosti 23 mpaka Agosti 25.

Kwa ratiba hiyo, ni kwamba Yanga na Azam zimedondokea kwenye timu za Ukanda wa Afrika Mashariki na wanachama wa CECAFA.

Endapo Yanga atafanikiwa kumuondoa kwenye michuano hiyo Vital'O, ataumana na mshindi kati ya Villa SC ya Uganda watakaocheza na Commercial Sports ya Ethiopia.

Wakati droo hiyo inatoka tayari timu za Tanzania zimeshaanza maandalizi ya kuelekea kwenye msimu mpya, ambapo Yanga ilianza mazoezi kwenye ufukwe wa Coco jijini Dar es Salaam, chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, ikitarajia pia kwenda nchini Afrika Kusini kucheza mechi ya Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs utakaopigwa Julai 28.

Azam FC yenyewe iko Zanzibar na leo inatarajiwa kukipiga na Zimamoto kwenye mchezo wa kirafiki, huku ikiwa kwenye maandalizi ya kuelekea nchini Morocco kuweka kambi.

Simba ambayo itasubiri hadi Septemba kucheza michuano hiyo ya CAF, nayo imeanza maandalizi ambapo tayari ipo nchini Misri kwenye jiji la Ismailia ikijifua kwa ajili ya michuano hiyo na Ligi Kuu.

Nipashe tunasema kwamba, Wawakilishi wa Tanzania wanatakiwa kutumia nafasi yao vizuri ya mandalizi kwa ajili ya kuimarisha vikosi vyao ili kuweza kupaata matokeo mzuri na hatimaye kufuzu hatua inayofuata.

Kama timu hizo zitakuwa zimaejipanga vizuri kama ambavyo viongozi wake wanavyojinasibu, basi Tanzania inaweza kuhushudia wawaikilishi wao wakiisonga mbele katika hatua kubwa zaidi ya mashindano hayo.

Sisi rai yetu ni kwamba sasa ni wakati muhimu kwa timu zote kufanya mazoezi kwa bidii ili kuhakikisha wanaiwakilisha vyema Tanzania kimataifa.

Haitosahi tu kufuzu hatua inayofuata, bali ni kuhakikisha timu zinafika mbali zaidi na ikiwezekana hata kubeba ubingwa wa mashindano waliyopo.