Chanzo wingi ajali bodaboda kijulikane

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 10:16 AM Jul 09 2024
Ajali  bodaboda.
Picha: Mtandao
Ajali bodaboda.

MAJERUHI 163,148 wa ajali za barabarani, walipokelewa katika vituo vya huduma za afya katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Dodoma na Kagera, ambayo ni maeneo vinara wa ajali.

Aidha, majeruhi 11,434 walihudumiwa kwenye hospitali 16 za rufaa katika kipindi cha kuanzia Juni 2023 hadi Juni mwaka huu, huku wale wa bodaboda wakiwa ni asilimia 61 ya majeruhi wote.

Hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. John Jingu ,wakati akizungumza katika semina na wadau wa usafirishaji inayofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.

Katika semina hiyo, katibu mkuu anawapa jukumu wadau hao, hasa madereva kuwa vinara wa kudhibiti ajali za barabarani ili kuokoa nguvu kazi ya taifa inayoteketea kwa ajali.

Ninadhani umefika wakati wa kutafuta chanzo cha ajali hizo, kwani kama ni elimu, imekuwa ikitolewa mara kwa mara, lakini pia inaelezwa kuwa  kwenye udereva wa bodaboda wamo pia wasomi.

Sasa kama wamo wasomi, wanakwama wapi kuzingatia kile ambacho wanafundishwa na kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria ya usalama barabarani ili wawe salama na abiria wao?

Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likikaa na madereva wa bodaboda vijiweni na kuwapa elimu, limekuwa likifanya hivyo mara kwa mara, lakini tatizo bado linaendelea.

Ninadhani ni vyema sasa chanzo cha wingi wa ajali za bodaboda kikaendelea kutafutwa ili kujua wanakwama wapi hadi wanajikuta wakisababisha ajali mara kwa mara na kupoteza maisha.
 
Katika mazingira hayo, wapo wengine wanapata ulemavu wa kudumu na kujikuta wakishindwa kufanya shughuli zao za kila siku na kubaki kutegemea watu wengine maisha yao yote.
 
Pamoja na hayo, madereva wenyewe wanaweza kujiongeza kwa  kuepuka tabia hatarishi kama kupita kwenye makutano ya barabara kabla ya kuruhusiwa na taa, 'kuovateki' kushoto, kubeba abiria juu ya mizigo au zaidi ya mmoja, kutovaa kofia ngumu na kuwa na haraka kila wakati.

Vilevile wanaweza kuacha kuendesha mwendo wa haraka hata katika barabara za mitaani na kutosimama kwenye alama za pundamilia au kuacha kupita pembeni mwa barabara kwa kukwepa matuta.

Madereva hao pia wanaweza kuacha kuendesha kwa haraka katika njia ya waenda kwa miguu au kuacha kuendesha wakiwa wamelewa, kwani baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kuendesha wakiwa wamelewa.

Kwa ujumla ni kwamba, zipo tabia nyingi hatarishi ambazo wakiziacha, usafiri wa bodaboda unawezaa kuwa salama kwao, kwa abiria wao na hata kwa waenda kwa miguu.

Inasikitisha kusikia kwamba, kwa mwezi Taasisi  ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI), inapokea majeruhi 700 wa ajali huku asilimia 60 wakiwa wamejeruhiwa kutokana na ajali za bodaboda.

Idadi hiyo inatajwa kuwa ni sawa na wastani wa majeruhi 23 wa ajali kila siku, huku ajali hizo zikiwapata madereva wa  bodoboda wenyewe, abiria au watembea kwa miguu wanaogongwa.

Binafsi njia nzuri ninayoiona ni kuendelea kuwapa elimu ihusuyo usalama barabara, lakini pia wale wasioizingatia, washurutishwe ili wawe salama na abiria au waenda kwa miguu.

Wasipuuzie elimu ambayo inatolewa kwao na Jeshi la Polisi  Kikosi cha Usalama Barabarani, kwani ndio inayoweza kuwaweka salama iwapo wataizingatia.

Ni kweli kwamba ajali haina kinga, lakini kwa jinsi wanavyoendesha vyombo hivyo bila kuzingatia sheria ya usalama barabarani, ni wazi ajali nyingine huwa wanazisababisha kwa kutokuwa makini barabarani.

Kwa mfano, wanazuiwa kubeba abiria zaidi ya mmoja, lakini wanabeba, wanafika makutano ya barabara, badala ya kusubiri taa ziwaruhusu, wao wanavizia ili wapite kabla na bila kuruhusiwa na taa.

Tabia hiyo inaweza kusababisha ajali, kwani chombo cha moto kinaharibika wakati wowote na kama dereva atakuwa amevizia ili kuvuka bila kuruhusiwa, anaweza kujikuta akiharibikiwa katikati ya barabara na hata kugongwa na magari kutoka upande ambao umeruhusiwa kupita.

Madereva wa bodaboda wasiwe chanzo na kumaliza nguvukazi ya taifa, wawe chachu ya kumaliza ajali, kwani Tanzania bila ajali barabarani inawezekana.