Viwanja vya soka viwe mtoko wa familia, isiwe kama adhabu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:35 AM Jul 13 2024
Uwanja wa kwa Mkapa.
Picha: Mtandao
Uwanja wa kwa Mkapa.

NILIKUWEPO kwenye Uwanja wa Manispaa ya Kinondoni, Mwenge jijini Dar es Salaam siku ya ufunguzi. Kulikuwa na mambo mawili, ufunguzi wa uwanja wenyewe pamoja na Kombe la Dar Port Kagame.

Moja kati ya mechi nilizoshuhudia katikati ya wiki hii ni ile ya Coastal Union dhidi ya Dekedaha FC ya Somalia, ikishinda kwa bao 1-0.

Ukiachalia mbali soka, lakini kilichonifurahisha ni jinsi mazingira ya watu waliokuwepo uwanjani humo.

Kama inavyojulikana Mwenge, licha ya kwanza kwa sasa ni eneo la Kibiashara, lakini pia ni lenye makazi ya watu kama ilivyokuwa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Watu waliokuwemo humo, wengi wao walikuwa ni wanawake wa umri mbalimbali, kuanzia wasichana wadogo mpaka akinamama.

Tena wengine walikuwa wamebeba watoto mgongoni na wengine walikuwa wamewashikilia na walikuwa bize kutazama soka.

Niligundua kuwa baadhi yao walikuwa hata hawajui timu gani zinacheza, lakini kwa sababu kuna mechi na mazingira mapya ya uwanja, walijongea.

Kilichoonekana ni kwamba pamoja na baadhi ya wafanyabiashara ya soko la Mwenge na maduka, lakini wengine hasa kinadada na kinamama walikuwa ni majirani wa eneo hilo.

Walikusanya familia na kusogea hapo kama mtoko. Ilionekana kama sikukuu hivi, kwani ndani mle mlikuwa mnauzwa vitu mbalimbali, viburudisho na vitafunwa, hivyo watu walionekana kuinjoi sana.

Niwapongeze sana viongozi wa Manispaa ya Kinondoni kwa kuujenga uwanja huo hasa maeneo ya kibiashara yaliyochanganyikana na makazi ya watu, kwani wameupeleka eneo la watu kabisa tofauti kama wangeujenga sehemu nyingine.

Uwanja huo ndiyo utakuwa uwanja wa nyumbani wa timu ya KMC, lakini pia hata klabu zingine zina fursa ya kuomba kuutumia.

Nikitoka hapo, nilipongeze pia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kwa kuamua kuukarabati uwanja wao wa Meja Jenerali Isamuhyo.

Wenyewe wanasema, pamoja na mambo mengine ya 'pitch', wanazungusha viti ili mashabiki wasipate tabu ya kusimama.

JKT na KMC wameonyesha dira kubwa kwa kujenga viwanja, hivyo kuwapa tamaa klabu zingine kufanya hivyo.

Tunahitaji viwanja vya aina hiyo hata kama ni vidogo, lakini viwe vingi kwa ajili ya kupunguza msongamano wa mechi mbalimbali za Ligi Kuu na michuano mingine.

Pamoja na yote bado nazikumbusha mamlaka za soka na wenye viwanja nchini kutengeneza mazingira ya kuvifanya kuwa rafiki kwa watazamaji wasijione kama wapo polisi au mahakamani.

Sina maana kuwa sehemu hizo ni mbaya, au zina matatizo, la hasha, ila haiondoi ukweli kuwa ndiyo sehemu ambazo watu wanakaa kwa uangalifu, heshima, adabu, woga na wasiwasi pia.

Na ndiyo sehemu ambazo raia huwa hawapendi sana kwenda, akifanya hivyo ujue amelazimika kweli, anakwenda kutafuta hali yake, au amepelekwa.

Mpirani hakutaki kuwa hivyo, badala yake ni sehemu ya burudani kama mtu aliyekuwa baa, disco, au kwenye ukumbi wa dansi au sherehe.

Kwa maana hiyo wamiliki wa viwanja, serikali na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), kuangalia na kutengeneza mazingira ya watu kupenda kwenda uwanjani, kama wanavyofurahia kwenda harusini, au kutazama ngoma, au shoo yoyote.

Zama za mtu akitaka kwenda uwanjani, anafikiria usalama, purukushani, mbwa mlangoni, njaa, kiu, zimepitwa na wakati.

Siku hizi tunaona hata akinamama na watoto wanakwenda uwanjani, hivyo wanapaswa kulindwa ili waendelee kuja na waongezeke.

Imefika wakati sasa viwanja vyetu kuwa kama vya nje, ambapo kuwe na vitafunwa, maji kwenye glasi nyepesi kuepuka warusha chupa, vyakula, vinywaji, kama vile watu wako 'pikniki' na si vitu hivyo kupatikana eneo la VIP tu.

Kwa kipindi hiki ambacho mashabiki wamekuwa wachache viwanjani, mazingira kama haya yatavutia mashabiki wengi ambao baadhi wanaweza kuingia si kutazama soka tu, badala yake kuinjoi kama mtoko hivi, kutokana na huduma zinazopatikana viwanjani.