Wachezaji Ligi Kuu msikimbie ushindani, pambanieni namba

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:00 AM Jul 15 2024
Nembo ya Ligi Kuu Bara.
Picha: Mtandao
Nembo ya Ligi Kuu Bara.

WAKATI usajili wa wachezaji ukiendelea nchini, kuna taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wanaondoka kwenye klabu wanazozichezea kwa kuhofia kupoteza namba.

Nimepenyezewa taarifa kuwa baadhi ya wachezaji wakiwamo hata wale ambao wanaichezea Timu ya Taifa, Taifa Stars au waliowahi kuichezea wanaondoka, wengine wakishinikiza kutaka kuondoka kutimkia timu nyingine ambako wanaamini watapata nafasi ya kucheza au hakuna ushindani mkubwa wa kugombea nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.

Hao ni wale ambao walikuwapo kwenye kikosi, lakini walipoona usajili wa wachezaji ambao wanadhani wanaweza kuwaletea changamoto, wao wanaona bora waondoke, lakini wapo ambao walikuwa wanashinikiza wenzao waondolewe ili wao wabaki, hii ni baada ya kuongezewa mikataba, wao wanaamua kuondoka.

Naweza kusema kuwa tabia hii ni ya kujishusha thamani kwa mchezaji mwenyewe na kutojiamini. Mimi ninavyojua moja ya tabia ya mchezaji soka wa ukweli ni kujiamini, kujiona anaweza kucheza popote pale, lakini pia kuwa na tabia ya kujitoa mhanga.

Mchezaji mpira mzuri ni yule ambaye ana uwezo wa kujitoa mhanga, au kuamia jambo gumu hata kama baadaye linaweza kumletea madhara.

Mfano mdogo wapo wachezaji walioamua kuacha hata ajira jeshini ili kwenda kujiunga na Klabu za Simba na Yanga, ili mradi tu kuweka masharti ambayo yatafidia kile ambacho alikuwa akipate akiwa huko. Na wengi wamefanya hivyo na wamefanikiwa, ingawa katika hilo ni lazima wawepo ambao hawakufanikiwa sana.

Mchezaji anayeogopa changamoto ya mchezaji wenzake kwenye namba ni kujiona kuwa yu dhaifu na kukubali kuwa hana uwezo wowote, badala yake amefika pale kwa bahati mbaya.

Nitoe mifano tu ya wachezaji ambao ama hawakuogopa kwenda timu zenye wachezaji mahiri, au waliokuwapo hawakulazimisha kuondoka baada ya kuletewa wachezaji wengine.

Simba iliwahi kumchukua Daud Salum 'Bruce Lee' ili kucheza beki wa kulia, iliyokuwa na Shaaban Baraza, Fibert Lubibisa alisajiliwa kama beki wa kushoto wakati Mohamed Kajole 'Machela' yupo, Yanga ilikuwa na beki wa kati Allan Shomari, lakini ilimleta Ishaka Hassan, kwenye kiungo ya kukaba ilikuwa na Issa Athumani, baadaye ikamsajili Athumani China, hakuna wakati ambao aliyekuwapo akaomba kuondoka kwa kumhofia anayekuja, wala anayekuja kuogopa kujiunga na timu kwa kuhofia kutopata namba.

Ni kwa sababu wote wao waliamini uwezo wao, kila mmoja aliamini kuwa kujituma kwenye mazoezi ndiko kutasababisha kupata namba.

Na kweli, vikosi vingine vya zamani vilikuwa na wachezaji ambao wanaweza kucheza namba moja, lakini uwezo ukawa unalingana na huwezi kutofautisha.

Simba ikawa na makipa, Mohamed Mwameja, Steven Nemes na Joseph Katuba, wote wakiwa kwenye kikosi kwa msimu mmoja, wakiwa ni makipa wa Taifa Stars na wote walikuwa wakiitwa.

Yanga ilikuwa na Joseph Fungo na Hamisi Kinye, makipa wa viwango vya juu kabisa, hakuna aliyemkimbia mwenzake, Pamba ikiwa na Madata Lubigisa na Paul Rwechungura.

Hii yote ni mifano michache inayoonyesha kuwa changamoto huwa hazikimbiwi bali zinakabiliwa na njia ni kujituma na kufanya kazi kwa bidii tu.

Nadhani hata wale ambao wanafundisha vijana kwenye 'akademi', waanze kuwafundisha  jinsi ya kuwa wavumilivu, kujituma na kutokata tamaa, kwani linaonekana ni jambo linaloanza kuwasumbua vijana wengi si kwenye soka tu, bali nyanja nyingi.

Vijana wengi wanapenda sehemu ambayo ni rahisi tu, hawapendi sana changamoto, ndiyo maana hupenda maisha ya raha na starehe na kutaka kupata vitu vingi vikubwa kwa muda mfupi bila kuvifanyia kazi ngumu.

Linapotokea jambo gumu kidogo ambalo linahitaji nguvu ya upambanaji, kujitoa au uvumilivu wanashindwa. Hiki ndicho kinachotokea kwenye soka wakati huu wa usajili. Mimi nawashauri wapambane ili kupata namba na si kukimbia, kwa sababu changamoto hazikimbiwi, bali inabidi kukabiliana nazo.