Ufaransa na Uingereza zinahimiza juu ya Ukraine kuhakikishiwa kuhusu kuendelea kwa mpango wa kupelekwa kikosi cha wanajeshi wa Ulaya nchini humo iwapo yatafikiwa makubaliano ya amani.
Baada ya mazungumzo yaliyohudhuriwa na takriban viongozi 30 hasa wa Ulaya na wa nchi wanachama wa jumuiya ya kujihami ya NATO yaliyofanyika mjini Paris siku ya Alhamisi, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameupongeza mpango ya kuwapeleka wanajeshi nchini Ukraine kutoka kwenye nchi kadhaa za Ulaya mara tu makubaliano ya amani kati ya Ukraine na Urusi yatakapoanza kutekelezwa.
Maelezo kamili juu ya mpangilio huo bado hayako wazi lakini inawezekana ukakamilika katika wiki zijazo. Maafisa wa ulinzi wa Uingereza na Ufaransa watatembelea Ukraine hivi karibuni ili kutathmini mahitaji ya ulinzi kiuhalisia, amesema rais Macron.
Rais wa Ufaranya katika mkutano na waandishi wa gabari baada ya mkutano na viongozi wenzake uliochukua muda wa saa tatu alisema "kutakuwepo na kikosi cha wanajeshi kutoka kwenye nchi kadhaa za Ulaya.”
Viongozi, waliohudhuria mkutano huo wa mjini Paris walikuwa ni Pamoja na Rais wa Ukraine Volodomyr Zelenskyy, Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni na Makamu wa Rais wa Uturuki Cevdet Yilmaz.
Hata hivyo Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ameeleza kwamba sio washirika wote wa bara Ulaya wanaokubaliana na mpango huo wa kupelekwa jeshi la Ulaya nchini Ukraine. Amesema hali hiyo ni kutokana na sababu mbalimbali za kila nchi binafsi.
Kwa wiki kadhaa sasa, Rais Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer wameungana katika juhudi za kuufanikisha mpango wa kuanzishwa " kikosi maalum" kwa ajili ya kuilinda Ukraine.”
Je, ni kwa nini nchi hizo zinataka uwepo mpango huo?
Ni kwa sababu Marekani iliifungia pazia Ulaya mapema mwaka huu kwa kuanzisha mazungumzo ya pande mbili kati yake na Urusi na ilisimamisha kwa muda msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Na kwa nchi za Ulaya, hofu kuu ni kwamba Rais wa Urusi Vladimir Putin anaweza kuthubutu kufanya mashambulizi zaidi nchini Ukraine, au mahala pengine barani Ulaya, kutokana nan chi hiyo kupewa masharti mepesi na Marekani.
CHANZO: DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED