JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, limekamata watu 123 kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya udhalilishaji wa watoto uliofanywa na vijana wadogo wenye umri wa miaka 14 na 18.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini, Unguja, watu wengine walikamatwa kwa makosa 837 ya usalama barabarani na kulipa faini mbalimbali kwa kipindi cha kuanzia Machi mosi hadi 25, mwaka huu.
Kuhusu waliodhalilisha watoto, akielezea tukio hilo Kamanda huyo amesema mtoto Yasini Seif (14) Mkazi wa Paje anatuhumiwa kumuingilia mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu, tukio lililotokea Machi 15, mwaka huu majiraya saa 7 mchana.
Tukio jingine lilitokea Machi 24, mwaka huu, eneo la Koboje Kinooni Wilaya ya Kati, mkoani Kusini Unguja kwa mtuhumiwa Nyambo Luponya (18) kumwingilia mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa.
Katika hatua nyingine, Jeshi hilo limesemalimeendelea kutoa elimu kupitia mradi wa poilisi jamii, dawati la jinsia na watoto pamoja na usalama barabarani
“Tunamafanikio mengi ikiwamo hukumu iliyotolewa Machi 5, mwaka huu na Mahakama ya Mkoa wa Mwera ambayo ilimuhukumu Hassan Ali Hassan (33) kulipa faini ya Sh. milioni 2 na fidia ya Sh. milioni 2 kwa makosa ya kusababisha kifo kutokana na uzembe na kupanda chombo cha moto ikiwa breki hazifanyikazi,” amesema.
Aidha, Machi 3, mwaka huu Mahakama ya Wilaya ya Mwera ilimuhukumu Jaffar Mwinyimvua (48) kifungo cha kutumikia kwenye Chuo cha Mafunzo kwa miaka mitano kwa kosa la wizi.
Pia Machi 3, mwaka huu, Mahakama ya Wilaya ya Mwera ilimuhukumu Bakari Ali Bakari (23) kutumikia Chuo cha Mafunzo kwa miaka mitatu na kulipa fidia ya Sh, 7,000 kwa kosa la wizi wa mazao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED