Wakazi sita wa Same kizimbani kwa kusafirisha kilo 518.57 za mirungi

By Grace Gurisha , Nipashe Jumapili
Published at 11:01 AM Mar 30 2025
Baadhi ya washtakiwa wanaotuhumiwa kusafirisha dawa kulevya aina ya mirungi wakisubiri kuingia kwenye chumba cha Mahakama kusomewa. mashtaka yao.
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya washtakiwa wanaotuhumiwa kusafirisha dawa kulevya aina ya mirungi wakisubiri kuingia kwenye chumba cha Mahakama kusomewa. mashtaka yao.

Wakazi sita wa Wilaya ya Same wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa jumla ya kilogramu 518.57.

Washtakiwa hao ni Nimkaza Mbwambo, Prosper Lema, Nterindwa Mgalle, na Stephanie Mrutu, ambao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ally Mkama.

MASHTAKA DHIDI YA WASHTAKIWA

Akiwasomea mashtaka, Wakili wa Serikali Julieth Komba alidai kuwa, Machi 21 mwaka huu, katika kijiji cha Rikweni, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, washtakiwa hao walikamatwa wakiwa wanasafirisha dawa hizo kwa nyakati tofauti.

Nimkaza Mbwambo anadaiwa kukutwa akisafirisha mirungi yenye uzito wa kilogramu 138.58.

Prosper Lema alikutwa akisafirisha kilogramu 113.29.

Nterindwa Mgalle alikamatwa na kilogramu 160.25.

Stephanie Mrutu alikutwa akisafirisha kilogramu 106.45.

Kwa kuwa upelelezi wa kesi hizo haujakamilika, mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Aprili 11 kwa ajili ya kutajwa, huku washtakiwa wote wakipelekwa mahabusu.

WAKAZI WENGINE WAWILI WA SAME PIA WAKAMATWA

Wakati huo huo, wakazi wawili wa Same, Dorisiana Mchome na Aisha Mbaga, wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Same wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha kilogramu 54.15 za mirungi.

Mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Hozza, washtakiwa hao walisomewa mashtaka yao ambapo ilidaiwa kuwa:

Dorisiana Mchome alikutwa akisafirisha kilogramu 17 za mirungi.

Aisha Mbaga alikutwa na kilogramu 37.15 za mirungi.

Wakili wa Serikali Michael Matowo alieleza kuwa upelelezi bado haujakamilika, na hivyo kesi imeahirishwa hadi Aprili 10, huku washtakiwa wakirudishwa mahabusu.

OPERESHENI YA DCEA SAME

Hivi karibuni, Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilifanya operesheni maalum wilayani Same, ambapo ekari 285.5 za mashamba ya mirungi ziliteketezwa.