Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, amewataka wananchi wa Wilaya ya Ludewa kuwa mabalozi wa uhifadhi wa misitu na mazingira, sambamba na kudhibiti matukio ya uchomaji moto holela kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
Chana ametoa wito huo leo, Aprili 18, 2025, wakati akifungua semina ya kujengeana uwezo kuhusu uhifadhi wa misitu, mazingira na mbinu za kuzuia na kudhibiti moto, iliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe.
“Misitu yetu inakumbwa na changamoto nyingi, zikiwemo uchomaji moto holela na ukataji miti hovyo kwa matumizi mbalimbali ya kibinadamu kama kuandaa mashamba, kuchoma mkaa au kuni kwa kupikia. Hivyo, ninyi mnaopata mafunzo haya muwe mabalozi wa kutoa elimu hii kwa wananchi mnaowaongoza ili kila mmoja wetu awe sehemu ya juhudi za uhifadhi wa mazingira,” amesisitiza Chana.
Ameeleza kuwa Wizara yake imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na changamoto hizo, ikiwemo kufanya doria za mara kwa mara, kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya moto na ukataji miti hovyo, pamoja na kugawa miche ya miti na mizinga ya nyuki kwa jamii zinazozunguka maeneo ya misitu.
Aidha, Chana amezitaka Halmashauri za Wilaya kuweka utaratibu wa kujadili kwa kina na mara kwa mara masuala yanayohusu uhifadhi wa misitu, vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla, kama njia ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kutunza mazingira kwa kuepuka ukataji miti na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amesema kuwa semina hiyo imekuja wakati muafaka na itaongeza uelewa kwa viongozi na wananchi kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira na misitu, hasa katika kuleta tija kiuchumi.
“Mafunzo haya yataleta matokeo chanya kwa wilaya yetu. Halmashauri tutaendelea kutoa ushirikiano kuhakikisha kuwa elimu hii inamfikia kila mwananchi na inaleta matokeo tarajiwa katika uhifadhi wa rasilimali zetu za asili,” amesema Thomas.
Semina hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Chama na Serikali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, Madiwani wa kata mbalimbali, wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na wadau wa uhifadhi kutoka wilaya hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED