Adaiwa kujiteka, akitaka mume wake atoe mil. 10 asitolewe mimba

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 02:34 PM Sep 26 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa.

Loveness Kisile (30), mkazi wa Mtaa Temeke, Kata ya Mhandu, Wilaya ya Nyamagana, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kwa tuhuma za kujiteka na kumshinikiza mumewe atoe shilingi milioni 10 ili asidungwe sumu ya kuondoa mimba ya mapacha watatu — jambo ambalo baadaye limebainika kuwa ni uongo.

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, wakati akizungumza jana na waandishi wa habari.

DCP Mutafungwa amesema Loveness anakabiliwa pia na tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwa mume wake na ndugu zake, akidai kuwa alitekwa na watu watatu wa jinsia ya kiume waliomlazimisha kulipa fedha ili wasimdhuru na kuondoa ujauzito wake.

Taarifa hizo, ambazo hazikuwa za kweli, zilitolewa Septemba 24, 2025, majira ya 05:30 usiku na kusababisha taharuki kwa mume wake, Hosea Lusigwa, na jamii kwa ujumla.

Mutafungwa amesema mwanamke huyo alidai kupitia simu kwamba watu hao watatu walimkuta wakiwa na pikipiki na gari, walimvalisha mfuko wa sulphate usoni ili wasimtambue na kisha walimpeleka kusikojulikana. Aidha, alidai kuwa wanataka shilingi milioni 10 na wasipotumiwa watamchoma sindano ya kuondoa mimba, na baadaye alimjulisha mume wake kuwa watoto wake mapacha watatu wamefariki.

"Alimsisitiza mumewe atume kiasi hicho cha fedha ili aachiliwe huru," amesema DCP Mutafungwa.

Jeshi la Polisi lilianza upelelezi mara baada ya kupokea taarifa hiyo na kumkamata Loveness akiwa salama na nguo zake akiwa amezichana mwenyewe, akiwa amejificha katika Mtaa wa Mecco, Kata ya Buzuruga, Wilaya ya Ilemela.

Hata hivyo, baada ya kufanyiwa vipimo vya kitabibu, ilithibitika kuwa mwanamke huyo hakuwahi kupata ujauzito. Alipohojiwa, alikiri kudanganya ili kuaminisha wakwe zake kuwa alikuwa mjamzito.