AG awafunda mawakili wa serikali

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 11:19 AM May 20 2025
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari
Picha: Thobias Mwanakatwe
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari, amewataka mawakili wa serikali kusikiliza na kutafuta suluhu kwa weledi malalamiko ya wananchi kuhusu masuala ya kisheria ili kuendeleza utawala wa sheria nchini.

Johari, alitoa rai hiyo jana wakati wa uzinduzi wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ngazi ya mkoa na wilaya mkoani hapa ulioambatana na Kliniki ya Sheria uliofanyika viwanja vya stendi ya zamani mjini hapa.

Alisema ili kudumisha amani na utengamano na kuchochea maendeleo kwa jamii na taifa, wananchi wanapaswa kusikilizwa na kutatuliwa changamoto zinazowakabili na serikali.

Johari, alisema Ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, hivyo wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kwao. 

"Moja ya njia inayotumiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwajibika kwa wananchi ni kutoa ushauri wa kisheria kwa ngazi ya mkoa na wilaya ndio maana mwongozo ulitolewa wa uanzishwaji kamati za ushauri wa kisheria za mkoa na wilaya," alisema Johari. 

Alisema lengo kuanzishwa kwa kamati hizo ni kurahisisha usimamizi wa utoaji wa ushauri wa kisheria kwa wananchi katika maeneo yao.

Akizungumzia kuhusu kliniki za kisheria, Johari, alisema zimelenga kuwaongoza wananchi katika taratibu za kupata haki zao pale zinapovunjwa au zinapoonekana kuelekea kuvunjwa.

Akizundua kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema itasaidia kupunguza mashauri na migogoro dhidi ya wananchi na serikali.

Dendego, alisema kamati hizo pia zitawawezesha mawakili wa Serikali kusimamia utawala wa sheria katika maeneo yao, kushirikiana na wadau kutatua kero za wananchi na kupunguza malalamiko yao ya kisheria.

“Naomba kukuahidi Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwa nitazisimamia kamati hizi kikamilifu ili ziweze kuwa na tija katika mkoa wetu," alisema.

 Alitoa wito kwa wananchi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi katika Kliniki ya Sheria bila malipo ili waweze kupata huduma za mirathi, ardhi, ndoa na ajira.