Husna aahidi maendeleo Chamanzi endapo atachaguliwa mbunge

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 01:51 PM May 20 2025
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Husna Sungura akionesha begi lenye fomu ya kuonmba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Chamanzi juzi mkoani Dar es Salaam.
Picha: Halfan Chusi
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Husna Sungura akionesha begi lenye fomu ya kuonmba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge Jimbo la Chamanzi juzi mkoani Dar es Salaam.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo, Husna Sungura, ameahidi kuleta maendeleo ya kweli kwa wananchi wa Jimbo la Chamanzi endapo atachaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo katika uchaguzi ujao.

Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa ubunge kupitia ACT Wazalendo, Husna amesema kuwa atahakikisha wananchi wa Chamanzi wanapata huduma muhimu kama umeme wa uhakika, maji safi na salama, pamoja na marekebisho ya barabara zinazowasumbua kwa muda mrefu.

“Kilichonisukuma kuwania ubunge ni kuona jinsi ambavyo serikali imeshindwa kutatua kero za wananchi kwa muda mrefu. Mimi ni mzaliwa na mkazi wa hapa, ninajua changamoto wanazopitia wakazi wa Chamanzi. Nitahakikisha kila mwananchi anafaidi keki ya taifa,” amesema Husna kwa msisitizo.

Ameongeza kuwa anapigania nafasi hiyo kwa nia ya kweli ya kuwahudumia wananchi na kuhakikisha kuwa kero ndogondogo zinazowakabili zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

“Nitapigania maendeleo ya Chamanzi kwa nguvu zote. Sitakuwa Mbunge wa maneno bali wa vitendo,” ameongeza Husna.