Chukueni tahadhari UVIKO-19 bado upo - Dk. Grace

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 01:14 PM May 20 2025
Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe.
Picha: Mtandao
Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe.

Mganga Mkuu wa Serikali Dk. Grace Magembe amesema ugonjwa wa UVIKO-19, umeendelea kuwepo kwa kiwango cha chini kama yalivyo magonjwa mengine ya mfumo wa njia ya hewa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.

Kupitia taarifa ya Dk. Grace aliyoitoa leo amesema vipimo vya maabara vimebaini kuongezeka na kupungua kwa virusi vya influenza hali ambayo imekuwa ikionekana pia katika miaka iliyopita na hujulikana kama 'Seasonal influenza’ na kwamba vipimo hivyo vimeonesha kuwa hakuna kirusi kipya.
 
Amebainisha kuwa tangu Februari hadi Aprili mwaka huu, ufuatiliaji wa virusi hivyo umeonesha ongezeko la visa vya UVIKO-19 kutoka wagonjwa wawili kati ya watu 139 waliopimwa sawa na asilimia 1.4 mwezi Februari, hadi wangonjwa 31 kati ya 190 sawa na asilimia 16.3 Machi.
 
“Mwezi Aprili mwaka huu kulipatikana wagonjwa 31 kati ya watu 185 waliopimwa sawa na asilimia 16.8, pia hali ya kuongezeka na kupungua kwa ugonjwa huo imekuwepo kila mwaka tangu kutangazwa kwa UVIKO-19 mwaka 2020,” amesema Dk. Grace.
 
Ameongeza kuwa kwa kipindi hiki ongezeko hilo linaonekana zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam. Na kwamba Wizara ya Afya inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa magonjwa ya mfumo wa njia ya hewa nchini na kutoa taarifa.