Majaliwa mgeni rasmi Tuzo za BMT 2024

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 01:00 PM May 20 2025
Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo za Baraza la Michezo la Taifa BMT  Mkumbukwa Mtambo katikati akizungumza na waandishi wa habari leo.
Picha: Shufaa Lyimo
Mwenyekiti wa Kamati ya tuzo za Baraza la Michezo la Taifa BMT Mkumbukwa Mtambo katikati akizungumza na waandishi wa habari leo.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwa mwaka 2024, itakayofanyika Juni 1 mwaka huu katika Ukumbi wa The Super Dome, Masaki, Dar es Salaam.

Hii itakuwa ni mara ya tatu kwa tuzo hizo kufanyika, baada ya zile za mwaka 2022 na 2023 ambazo zilivutia zaidi ya washiriki 700 kutoka sekta mbalimbali za michezo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo, Profesa Mkumbukwa Mtambo, amesema maandalizi kwa ajili ya hafla hiyo yamekamilika kwa kiwango kikubwa huku mchakato mzima ukitarajiwa kwenda kwa weledi na ubora wa hali ya juu.

Profesa Mtambo amesema tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini na kuenzi mafanikio ya wanamichezo na timu zilizofanya vizuri mwaka 2024, huku akieleza kuwa mwaka huu wameongeza vipengele viwili vipya ili kuifanya hafla hiyo kuwa ya kipekee.

Baadhi ya vipengele vinavyowaniwa ni pamoja na:

  • 👑Mwanamichezo Bora wa Kiume na wa Kike
  • 👑Mwanamichezo Bora Kijana (wa Kiume na wa Kike)
  • 👑Mwanamichezo Bora kwa Watu Wenye Ulemavu
  • 👑Timu Bora ya Taifa ya Mwaka (Wanaume na Wanawake)
  • 👑Timu Bora ya Klabu ya Mwaka
  • 👑Kocha Bora wa Mwaka (Kiume na Kike)
  • 👑Mwanamichezo Bora kutoka Mashuleni
  • 👑Mwamuzi Bora wa Mwaka
  • 👑Mwanahabari Bora wa Michezo
  • 👑Mwanamichezo Nguli wa Zamani
  • 👑Mchezaji Bora wa Chaguo la Watu
"Mwaka huu tumekuja tofauti. Tumeongeza thamani ya tuzo kwa kuwatambua wanamichezo nguli wa zamani pamoja na kuweka kipengele cha mchezaji bora wa chaguo la watu," amesema Profesa Mtambo.

Ameeleza kuwa kupitia kipengele hicho, wadau na wananchi watapata nafasi ya kupiga kura kumchagua mchezaji bora wanayemuona anastahili, hatua inayoongeza ushiriki wa jamii katika kuthamini mafanikio ya wanamichezo nchini.

Aidha, Kamati hiyo itashirikiana na vyama na mashirikisho ya michezo ya kitaifa katika mchakato wa kutambua na kuchagua washindi wa tuzo, kwa kuzingatia ushindani na mafanikio ya mwaka 2024 katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.