Msuya anakumbukwa kwa mambo mengi hasa kutokana na mambo mengi yakiwamo mabadiliko ya kiuchumi ndani ya serikali. Wakati wa awamu ya kwanza, Tanzania haikuwa na maelewano mazuri na mashirika ya kimataifa ya fedha hasa Benki ya Dunia na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFM).
Kutokana na hali hiyo, serikali ya awamu ya pili ilianza mazungumo kuhusu mageuzi ya sera za kiuchumi na Msuya ndiye aliyekuwa mstari wa mbele katika mchakato huo.
Msuya pia ndiye aliyeibeba sura ya Mwanga, kwa maana ya wilaya, jimbo la uchaguzi na Dayosisi ya KKKT Mwanga. Vitu vyote hivyo vina mchango mkubwa sana kutoka kwake kutokana na uthubutu wake pamoja na kuwapo kwavyo na kustawi. Kutokana na kuwa mstari wa mbele wa vitu hivyo, alijipatia sifa nyingi na hata kuitwa ‘Baba wa Mwanga’.
Awali, Mwanga ilikuwa sehemu ya wilaya ya Same ikijulikana kama wilaya ya Upare mwaka 1961 lakini ilianzishwa rasmi kuwa wilaya Septemba Mosi 1979. Kabla ya hapo iligawanywa kutoka jimbo la Upare (Same ya sasa) na kuwa Mwanga, Msuya akiwa mbunge wake kwa kwanza.
Kuwapo kwa jimbo na wilaya, kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na jitihada zilizofanywa na Msuya kitaka eneo hilo kujitegemea. Kuwapo kwa eneo hilo la kiutawala na uchaguzi, kuliibua kasi kubwa ya kimaendeleo kama vile barabara na umeme huku Msuya akilalamikiwa kuwa anapendelea nyumbani kwake kiwa kuweka miundombinu hiyo hadi kwenye migomba lakini hakujali.
Licha ya madai hayo kutoka kwa baadhi ya wapinzani wa kimaendeleo, Msuya alikaa kimya na kuendelea na mipango yake kwa ajili ya jimbo na wilaya ya Mwanga kwa kuendelea kupeleka miradi ya maendeleo hasa maji, barabara na umeme kwa wananchi wa maeneo kama Mwanga yenyewe, Usangi na Ugweno.
Hayo si kwamba aliyafanya akiwa Waziri Mkuu (1980 – 1983) na Makamu wa Kwanza wa Rais (1994-1994) bali hata alipokuwa Waziri wa Fedha na Waziri wa Viwanda na Biashara kwa vipindi tofauti tangu serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere na awamu ya pili chini ya Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Wako pia waliobeza kuwa wilaya ya Mwanga ilianzishwa kwa shinikizo la kisiasa kutoka kwa kiongozi huyo kwa sababu kama halmashauri ilikuwa haijitoshelezi hata kwa mapato ya ndani. Msuya hakujali.
Licha ya kupeleka maendeleo katika jimbo na wilaya, matokeo ya Mwanga kuwa Dayosisi ya KKKT ina mchango kutoka kwa Msuya. Tangu Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Msuya alisimamia kidete kuwapo kwa dayosisi hiyo lakini alipata upinzani kutoka kwa baadhi ya viongozi wa KKKT makao makuu kuwa ilikuwa haijatimiza vigezo.
Hata hivyo, hatimaye Mwanga ilipata baraka za kuwa dayosisi katikati ya miaka ya 2010 na sasa ina takriban miaka 10 tangu kuasisiwa kwake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED