MWENYEKITI wa Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga, Mibako Mabubu amekabidhi maguni ya mahindi 82 kwa ajili ya chakula kwa shule za msingi na sekondari kata ya Chela, kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula ili kuboresha ufaulu wao.
Akikabidhi magunia hayo leo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Rose Manumba, Mibako amesema, umeungana na wazazi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula shuleni na itasaidia kupunguza utoro na kuongeza ufaulu katika mitano yao ya mwisho.
Aidha amewataka watendaji wa kata kusimamia kwa karibu utekelezaji wa agizo hilo na kutoa taarifa za kila shule ili kujua namna utekelezaji unavyofanyika. Baadhi ya shule hazitoi chakula, jambo linalochangia utoro wa wanafunzi, na kusisitiza wazazi kuendelea kukumbushwa umuhimu huo.
“Kati hii ina shule 12 kati yake sekondari ni tatu na kila shule itapata chakula kulingana na wingi wa wanafunzi, mwaka juzi nilitoa maguni ya mahindi 68, mwaka jana 73 na mwaka huu 82 na ninatoa kuunga mkono michango ya wazazi pale wanapoishia”Ameongeza Mibako.
Awali akipokea chakula hicho, Mkurugenzi Manumba amesema suala la lishe katika shule za msingi na sekondari ni suala la kitaifa hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula ili kuimarishga afya lakini pia kuongeza ufaulu na kupunguza daraja sifuri.
Aidha amewataka wazazi na walezi wahakikishe watoto wao wanafika shuleni pamoja na kusimamia maadili ya watoto wanapokuwa majumbani huku walimu wakitakiwa kutumia chakula hicho kwa malengo yaliyokusudiwa ili kileta tija nasio kwenda kukiuza.
Manumba amesema watendaji wa kata wamepewa dhamana ya kuongoza katika maeneo yao na wanajukumu la kusimamia utekelezaji wa agizo la upatikanaji wa chakula mashuleni, kwa kutumia njia shirikishi kwa jamii ili kuhakikisha kila mtoto anapata chakula shuleni pasi kukosa masomo.
Aidha amesema, mpango huu unalenga kupunguza njaa na utoro mashuleni, na umeungwa mkono na viongozi mbalimbali wa serikali na jamii na halmashauri inaendelea na juhudi za kuboresha lishe na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi ili kufikia malengo ya kitaifa ya elimu bora kwa wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED