"Kuna mambo mengine sikutaka kuyasema kwa sababu nina uwezo mkubwa sana wa kupuuza lakini nimechokonolewa sana na baadhi ya watu kiasi ambacho inawezekana kuna baadhi ya watu mkachanganywa. Kwahiyo kwasababu nimelazimishwa, mengi nitapuuza, nitasema walau moja, naomba mnikubalie.
"Kuna mtu mmoja ambaye amekuwa akijinadi siku nyingi anasema wakati anaenda kwenye 'SendOff' alitumia koti langu mimi mtoto wa muuza uji. Lakini leo hii anadiriki kufikia kusimama mahali anasema eti Gambo ameumiza watu wengi.
"Leo nataka niwaulize hivi mimi na yeye nani ameumiza watu wengi katika nchi hii? hivi mnapajua Dar es Salaam ninyi? nendeni mkatafute habari zake kule hata kumsalimia mtaogopa," amesema Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo, wakati akizungumza na wananchi wa Arusha katika mkutano wake wa hadhara.
Pia amesema anataka popote alipo bila kuweka wazi jina halisi la anaemzungumzia, kwamba wamuambie mikono yake ni safi! Na hana changamoto yoyote na hajamuumiza yeyote badala yake amesaidia watu wengi kote alipopita.
"Nimesaidia watu wenye ulemavu, tumewapatia viti mbalimbali kwaajili ya kuwasaidia, tumewasaidia watu kupata miguu bandia ambao hawakutarajia kupata ulemavu, tumesaidia vituo vya yatima, tumesaidia kila mahali. Mwambieni hayo ni matendo mema hakuna hata moja la kumuumiza mtu," amesema Gambo.
Ifahamike kuwa siku chache zilizopita kumekuwa na hali ya kurushiana maneno ya vijembe kati ya mbungr huyo Gambo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda. Gambo amesema "Nimeamua nisema kwasababu amesema eti nenda kwa wananchi wa Arusha, nenda kawaombe radhi, wananchi wa Arusha nimewahi kuwakosea?".
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED