Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu, leo ametangaza kwamba uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa miaka minne mfululizo (2020/21–2023/24) unaonyesha wazi kuwa Serikali ya CCM imeshindwa kusimamia fedha za umma na imejaa uzembe, ubadhirifu na ukosefu wa uwajibikaji.
Akizungumza kutoka Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar es Salaam leo, Dorothy alisema kuwa hoja za ubadhirifu zenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 2.56 zimekuwa zikirudiwa kila mwaka bila hatua madhubuti kuchukuliwa. Alibainisha kuwa fedha hizo zingetumiwa kwa tija, zingeweza kupunguza kasi ya kuongezeka kwa deni la taifa na kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
"Watanzania wamechoka. Miaka minne ya Rais Samia ni miaka ya fungulia mbwa. Tunapaswa kutumia mwaka 2025, kuonesha hasira zetu dhidi ya wazembe, mafisadi na wababaishaji wa Taifa letu; ambao ni CCM." amesema Dorothy.
Dorothy amewataka Watanzania kutumia mwaka huu wa uchaguzi kuonyesha hasira zao dhidi ya ufisadi wa CCM kwa kuichagua ACT Wazalendo chama ambacho kina dhamira ya dhati kusimamia rasilimali za taifa kwa haki, tija na maendeleo ya wengi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED