SERIKALI imetoa vifaa vya kisasa vya utafiti wa maji chini ya ardhi,huku ikitoa maagizo kwa mamlaka za maji kuhakikisha zinafanya tafiti za kina ili kuhakikisha watanzania wote wanapata maji.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Maji,Juma Aweso katika hafla ya makabiadhiano ya vifaa hivyo vyenye thamani ya sh bilioni 5.2,kwa mabonde nane ya Maji hapa nchini.
Aweso amesema vifaa hivyo vya kisasa ambavyo vimenunuliwa kwa za fedha za Uviko 19,vinakwenda kumaliza changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini ambayo bado hayajafikiwa na maji kwa asilimia inayotakiwa.
Kutokana na hilo,ameziagiza mamlaka hizo kuhakikisha vijiji zaidi ya 1,500 ambavyo vilikuwa havina maji kuhakikisha vyote vinapata maji ili kutimiza azma ya serikali ya kumtua ndoo mama kichwani.
"Sasa hivi natarajia kutosikia kikwazo chochote kutoka kwa wataalam wa sekta za maji kuhusu upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali hususani vijijini na baadhi ya maeneo mjini kafanyeni tafiti za kina kupitia vifaa hivi,serikali imetoa vifaa vya kisasa ambavyo vinafanya utafiti umbali mrefu kwenda chini hivyo maji yatapatukana,"amesema Aweso.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji DK George Lugomela amesema vifaa hivyo vitatumika kuchunguza mipasuko kwenye matabaka ya miamba inayoweza kuhifadhi maji,kuchunguza uwepo wa maji kwenye.matabaka ya miamba.
Vifaa hivyo pia vitawasaidia wataalamu wa sekta ya maji kupima uwepo wa maji kwa njia tatu lakini pia kina uwezo wa kwenda kuchunguza maji umbali wa mita 1,000,huku vifaa vingine vikitumika kupima kina cha maji kwenye visima virefu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED