Katibu wa BAWACHA Kilimanjaro aondoka CHADEMA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:42 PM May 11 2025
news
CHADEMA
Grace Kiwelu

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum na Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa BAWACHA Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Kiwelu ametangaza kuachana na Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA).

Kiwelu ambaye ni Mwenyekiti Kamati ya Fedha wa Kanda ya Kaskazini na ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya BAWACHA Taifa, amesema uamuzi huo unatokana na mfululizo wa manyanyaso na matusi kutoka kwa uongozi wa sasa licha ya nguvu kubwa waliyotumia kukijenga chama hicho. 

Grace amesema:Nimekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu na nimejiunga na chama hiki tangu mwaka 1992 nikiwa binti na leo nazeeka ndani ya chama, lakini leo (Mei 11,2025) nimesimama mbele yenu kwa maumivu makubwa kwasababu nitasema mwishoni ninaenda wapi. 

“Chama changu nilikipenda sana na nilikitumikia kwa moyo wa dhati, tulizunguka nchi nzima hii kuijenga CHADEMA, tulikuwa tunazunguka na Mwenyekiti Mstaafu, Freeman Mbowe kuhakikisha kinaenea Tanzania nzima. 

“Tulifanya ziara wakati huo tukiwa wabunge watano tu, mimi nikiwa mbunge pekee mwanamke kuzunguka nchi hii tukiwa na fuso, tunaweka viti, meza, spika. 

“Tunazunguka na hatuna mwanachama hata mmoja huko tunapoenda. Tukifika tunashusha viti, tunafunga Spika, tunahutubia miti na watoto. Leo namshukuru Mungu tumefika hapa. 

“Lakini badala ya kuvuna heshima, tunavuna matusi. Tulishauri chama kwa nia njema kwamba tunahitaji ‘reforms’ (mabadiliko) ndio lakini tusizuie uchaguzi. 

“Unawezaje kuzuia uchaguzi wakati wewe sio mshirika wa uchaguzi? Tunafanyaje mikutano wakati tumeshasema tunaenda kuzuia uchaguzi? Tunauzuiaje uchaguzi?, wakasema tutazuia kwa maandamano. 

“Leo wananchi wangu wa Vunjo niwaambie tunaandamana kuzuia uchaguzi, tunaanzia wapi tunaishi wapi? Wazee wangu wa Vunjo na vijana,tunaanzia wapi? 

“Maandamano tunayofanya ama vijana wanaoandika leo kutukana baba na mama zao kwenye mitandao hutowaona kwenye maandamano. Na niwaombe sana wananchi wangu wa Vunjo, nilikuwa mmoja wa G55 kwasababu ninawajali, ninawaheshimu na ninawapenda. 

“Leo Viongozi wanaona matusi hawakemei, kosa ni kumuunga mkono Mbowe na nilimuunga mkono kwasababu ya mageuzi makubwa aliyoyafanya ndani na nje ya chama chetu. Bila Mbowe tusingekuwa na CHADEMA hii ya leo. 

 “Ana haki ya kupongezwa, kwahiyo mimi nimechukua maamuzi tayari kwamba leo ninafikia mwisho wa kuwa mwanachama wa ChADEMA, niwashukuru viongozi wangu wa BAWACHA kwa kuniunga mkono na tutakwenda pamoja kuendeleza mapambano ya haki za wanawake na wananchi wetu, kuyafikia malengo tuliyokuwa tumetegemea kuyafikia." Grace.