Mwenyekiti wa Halmashauri ya Msalala, Mibako Mabubu, amekabidhi magunia 82 ya mahindi kwa ajili ya chakula kwa shule za msingi na sekondari zilizopo Kata ya Chela, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe shuleni ili kuboresha ufaulu na kupunguza utoro.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Rose Manumba, Mibako amesema ameshirikiana na wazazi katika juhudi za kuhakikisha wanafunzi hawakosi chakula shuleni. Amesisitiza kuwa lishe bora ni haki ya kila mtoto na nyenzo muhimu katika kukuza ufaulu wa wanafunzi.
“Kata ya Chela ina jumla ya shule 12, kati ya hizo shule za sekondari ni tatu. Kila shule itapatiwa chakula kulingana na idadi ya wanafunzi. Mwaka juzi nilikabidhi magunia 68, mwaka jana 73, na mwaka huu nimeongeza hadi 82. Hii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za wazazi na jamii kwa ujumla,” alisema Mibako.
Aidha, amewataka watendaji wa kata kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango huo, pamoja na kutoa taarifa sahihi kuhusu hali ya utoaji wa chakula katika kila shule. Aliongeza kuwa baadhi ya shule bado hazijaanza kutoa chakula jambo ambalo linaathiri mahudhurio na maendeleo ya kitaaluma ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri, Rose Manumba, alipokea msaada huo kwa niaba ya halmashauri na kupongeza juhudi za Mhe. Mibako. Alisema kuwa suala la lishe shuleni ni ajenda ya kitaifa, na ni wajibu wa kila mzazi, mlezi na kiongozi kuhakikisha watoto wanapata chakula wakiwa shuleni.
“Lishe bora shuleni huongeza umakini wa mwanafunzi darasani, hupunguza utoro, na kuchangia ufaulu wa wanafunzi. Ni wajibu wetu kama jamii kushirikiana kwa karibu kuhakikisha watoto wetu hawakosi mlo shuleni,” alisema Manumba.
Ametoa wito kwa walimu kutumia mahindi hayo kwa matumizi yaliyokusudiwa na si vinginevyo, huku akisisitiza uadilifu na uwajibikaji. Pia aliwataka wazazi kuendelea kuwahimiza watoto kuhudhuria shule na kuzingatia maadili hata wakiwa nyumbani.
Mpango huo unaelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada za halmashauri ya Msalala katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufanikisha malengo ya kitaifa ya elimu bora kwa wote.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED