NMB yaandika historia ikishinda tuzo sita ikiwemo ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika”

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:59 PM May 12 2025
NMB yaandika historia ikishinda tuzo sita ikiwemo ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika”
Picha: Mpigapicha Wetu
NMB yaandika historia ikishinda tuzo sita ikiwemo ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika”

Benki ya NMB inatangaza mafanikio ya kihistoria ya ushindi wa tuzo sita za kimataifa kutoka kwa majarida mawili mashuhuri duniani - jarida la Euromoney linalochapishwa London, Uingereza, na Global Banking & Finance Magazine lenye makao makuu yake New Jersey, Marekani.

Ushindi huu mkubwa unaashiria kutambuliwa kwa ubora wa huduma, ubunifu na mchango wa Benki ya NMB katika kuchangia maendeleo endelevu ya kiuchumi nchini.
 
Miongoni mwa tuzo hizo ni ile ya heshima ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika” inayodhibitisha mafanikio na maendeleo makubwa ya NMB na tasnia nzima ya fedha nchini.
 
Tuzo ya “Benki Bora kwa Uendelevu Barani Afrika”, iliyotolewa hivi karibuni jijini London katika hafla ya Euromoney Private Banking Awards 2025, imeweka historia kwa kuwa ya kwanza kutolewa kwa Benki ya Kitanzania.. Hii ni hatua kubwa ya kutambua mchango wa Tanzania katika eneo nyeti la uendelevu, ambalo lina umuhimu mkubwa katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na mazingira duniani kote.
 
Ushindi huu unadhihirisha jitihada za Benki ya NMB za kuongoza mabadiliko na dhamira yake ya dhati za kuyafanya masuala ya mazingira, jamii na utawala bora (ESG) kuwa sehemu ya msingi katika shughuli zake za kiutendaji na dira yake ya kimkakati.
 
Benki ya NMB pia ilinyakua tuzo mbalimbali kama kinara wa kitaifa katika sekta ya benki kutoka kwa majarida hayo mawili kama ifuatavyo:
 

Euromoney:
● Benki Bora ya Uendelevu Tanzania
● Benki Bora ya Wateja Maalum Tanzania (kwa mwaka wa tatu mfululizo)
 
Global Banking and Finance Magazine:
● Benki Salama Zaidi Nchini Tanzania
● Kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii Tanzania 2025
● Afisa Mtendaji Mkuu Bora wa Benki Tanzania 2025 (Tuzo hii ilitolewa kwa CEO Ruth Zaipuna)
 
Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB,Ruth Zaipuna alipongeza kwa tuzo hizo huku akisema : “Ni hatua ya kihistoria kwa tasnia ya fedha nchini. Aidha, alisisitiza kuwa tuzo hizi ni hatua muhimu katika kuisaidia Tanzania kujipambanua kama kiongozi wa kikanda wa ufadhili endelevu na utoaji wa huduma bora za kifedha.
 

“Ni heshima kubwa kwetu kutambuliwa na Euromoney na Global Banking & Finance Magazine kwa uongozi wetu katika Ufadhili Endelevu na Huduma kwa Wateja Maalum,” alisema Zaipuna. “Tuzo hizi sita ni ushahidi wa juhudi na kujitolea kwa wafanyakazi wetu,, imani kubwa ambayo wateja wetu wameendelea kutuonesha, na dhamira thabiti tuliyonayo ya kujenga mustakabali wa ustawi, ujumuishaji, na maendeleo endelevu kwa nchi yetu.”

 

"Sisi kama Benki ya NMB, uendelevu si tu ni wajibu wa kibiashara bali ni hitaji la kimkakati linalochangia uimara wa biashara, kuchochea ubunifu, kuongeza ushindani, na kuhakikisha upatikanaji wa thamani ya kudumu. Kwa kuufanya  uendelevu kuwa kiini cha mkakati wetu wa biashara, tunawahakikishia wadau wetu thamani ya kudumu na kuwa na athari chanya kwa jamii tunazozihudumia."

 
Benki ya NMB pia imepata heshima ya kutambuliwa kama Benki Salama Zaidi nchini Tanzania kutokana na dhamira yake thabiti katika maendeleo ya kiteknolojia na rasilimali watu.

 
“Tuzo hii ni matokeo ya moja kwa moja ya uwekezaji wa kimkakati katika ubunifu na hatua madhubuti za usalama wa mtandao, hali inayowezesha uwepo wa mazingira ambayo yanafanya wateja zaidi ya milioni 8.6 kuwa na imani na uimara wa kifedha wa Benki ya NMB na usalama wa fedha zao.

 

"Tumejidhatiti kukuza uwezo wetu na kuhakikisha ufanisi wa kifedha wa kudumu, tutaendelea kuwekeza katika teknolojia na rasilimali watu ili kukidhi mahitaji anuwai ya wateja wetu tunaowathamini kwa moyo wote," alihitimisha Zaipuna.

 

Akizungumzia tuzo hizo, Mhariri Mkuu wa Euromoney, Louise Bowman, alisema, “Benki ya NMB imedhihirisha kuwa taasisi kinara wa maendeleo endelevu nchini Tanzania na barani Afrika kupitia mipango yake ya kimkakati inayozingatia uwiano wa uwajibikaji wa kimazingira, athari chanya kwa jamii, na ukuaji wa kifedha.”

 
Tuzo hizi zinabainisha dhamira ya Benki ya NMB katika uendelevu wa mazingira na jamii, sambamba na kutoa masuluhisho bora ya kifedha yenye viwango vya kimataifa, ambayo yanawawezesha wateja na kuchochea maendeleo jumuishi ya kiuchumi. Kutambuliwa huku ni uthibitisho wa maono ya kimkakati ya Benki ya NMB katika kuendeleza Ukuaji Jumuishi na Maendeleo Endelevu, huku ilipanua wigo wa upatikanaji wa huduma za kifedha kwa Watanzania wote.
 
Benki ya NMB inaendeleza kwa dhati dhamira yake ya kuzingatia viwango vya juu kabisa vya ubora wa huduma za kibenki, kuendeleza ubunifu, na kuchangia kikamilifu katika maendeleo endelevu ya Tanzania chini ya uongozi wa ushindi wa Zaipuna.