FUKUTO ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( CHADEMA) linazidi kushika kasi baada ya jana viongozi wengine kutoka kanda nane Tanzania Bara kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho.
Viongozi hao ni kutoka Kanda ya Kati, Serengeti, Victoria, Pwani, Kusini, Kaskazini. Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam kwa niaba ya wenzake, aliyekuwa Mwenyekiti CHADEMA Kanda ya Kati, Jingu Jackson alisema sababu kuu ya wao kujivua uanachama ni chama hicho kimepoteza uelekeo.
Jingu alisema hali ya siasa ndani ya chama hicho kwa sasa ni mbaya kwa sababu viongozi wapya walioingia madarakani wameonesha kukiuka kwa falsafa na kanuni za chama.
Alisema tangu viongozi hao walipoingia madarakani wamekuwa wakitumia mamlaka yao vibaya kwa kuwakandamiza wengine hususani waliokuwa wakimuunga mkono aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe.
Jingu alisema kitendo cha viongozi wa CHADEMA kutangaza kususia kusaini kanuni za uchaguzi kimeisababishia hasara kubwa chama hicho kwa kuzingatia mlengo namba moja wa chama chochote cha siasa duniani ni kushiriki Uchaguzi Mkuu.
Alisema: " Hali ya kisiasa ndani ya chama ni mbaya sana. Chama badala ya kwenda mbele sasa hivi kinarudi nyuma. Kila siku migogoro na matusi ambayo hayakijengi chama. Kila siku wanamtukana Freeman Mbowe".
Jingu alisema kitendo cha kukiuka madhumuni ya chama na Katiba viongozi hao wanastahiri kufukuzwa uanachama kwa sababu wanalengo baya ya kukiangamiza chama ambacho kilishakuwa imara na thabiti kwa watanzania.
Alisema kitendo cha Chadema kutoshiriki uchaguzi imewanyina watanzania haki ya kuwa na washiriki katika vyombo vya maamuzi ikiwemo bungeni. Jingu alisema viongozi wa sasa wa CHADEMA wamekuwa wakitoa ahadi za uongo na zisizotimizwa tangu walipoingia madarakani ikiwemo ahadi ya kutoa Sh. 100,000 kila mwezi katika majimbo ya uchaguzi, kwamba hadi sasa hakuna pesa yoyote iliyotolewa.
Jingu alisema: "Leo sisi ambao tulikuwa ni viongozi wa chama kutoka kanda nane tumeamua kujivua uanachama na vyeo vyetu vyote, kwamba tutaendelea kuwa watanzania na hatutakuwa na chama chochote".
Viongozi waliotangaza kujiondoa CHADEMA ni Emma KImambo aliyekuwa mweka hazina Kanda ya Kaskazini, Gimbi Masaba ( Makamu Mwenyekiti Serengeti), Bazir Lema (Katibu wa chama Mkoa wa Kilimanjaro, Katibu wa Mafunzo).
Wengine ni Hadija Mwago ( Mwenyekiti wa Bawacha Mbagala), Aboubakar Mlope (Mweka hazina Kanda ya Kaskazini, Katibu wa Bavicha Kanda ya Kusini), Magreth Mlekwa ( Katibu wa Bawacha Kanda ya Nyasa), Ester Filano ( Katibu wa Bawacha Victoria).
Wengine ni Jackline Kimambo ( Katibu wa Kamati ya Mafunzo Kanda ya Kaskazini), Stuart Ernest (Ofisa wa Chadema Kanda ya Kusini), Doris Mbatili (Katibu wa Mafunzo Kanda ya Victoria), John Lema (Ofisa wa Oganizesheni na Mafunzo Kanda ya Kaskazini).
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED